JIBU: Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho. Moja katika masharti ya kukamilishwa kabla ya kutolewa Zakaah ni mali iliyopo ipitwe na Hawl (mwaka wa Kiislamu). Pia mali iwe ni yenye kumilikiwa wakati wa kutolewa Zakaah umilikaji uliotimia (complete possession) na tayari imeshatimia au kuvuka kiwango (Nisaab). Na Zakaah itahesabiwa pale mwisho wa Mwaka kwa kila kilichopo wakati wa kufunga mahesabu ambacho tayari kiko ndani ya milki ya mwenye kutoa Zakaah. Hivyo kufafanua mas-ala yako ni kama ifuatavyo: Shurti la kupitiwa na mwaka Katika mali ya biashara ikiwa mwanzo wa mwaka yaani (Shawwaal kwa mfano uliotuletea) mali iliyopo tayari imefikia Nisaab (sawa na gramu 85 za dhahabu safi) basi ikimalizika mwaka (Ramadhaan) tunaangalia bidhaa iliyopo na pesa zilizopo Benki ambazo tayari zimo kwenye milki yenu na kisha kutoa Liabilities zote kama (madeni, malipo n.k) na kitakachobaki ndicho kitahesabiwa kutolewa. Bidhaa hutiwa thamani kwa mujibu wa thamani iliyopo (market value). Tanbihi: Si lazima kuangalia nini kimeingia na kipi kimetoka wakati biashara inaendelea kinachotazamwa ni mwanzo wa mwaka je mali ilifikia kiwango? Na mwisho wa mwaka mali iliyopo yote ndiyo itakayotiwa katika hesabu ya Zakaah. Na kama mali yenyewe bado ni bidhaa basi gharama/thamani inayouzwa (market value) ndiyo kigezo cha kuangalia na si gharama iliyonunuliwa (buying price). Hapa itategemea ikiwa mali hii katika mzunguko wake wa kibiashara haitopungua kiwango. Hivyo mtaangalia bidhaa zenu zilizoko kwenye ghala kama zingeliuzwa wakati ule zingekuwa na gharama gani (inawezekana gharama hizi kuzidi au kupungua na bei iliyonuniliwa). Na hapa tutawekea jedwali ndogo ya kuainisha vipi katika ulivyovitaja vitapaswa kutolewa/kutotolewa Zakaah MALI/BIDHAA/LIABILITIES ZINATOLEWA HAZITOLEWI BIDHAA ZILIZOPO DUKANI NA GHALANI Ni bidhaa yenye kuongezeka na ipo kama ni mali PESA ZILIZO BENKI NA MKONONI Ni mali MZIGO TUMESHANUNUA BADO UPO NJIANI Kwa sababu bado hamjaumiliki kikamilifu(complete possession) BIMA Si sehemu ya matumizi (ingawa inategemea na BIMA yenyewe, pia na nchi kama ni lazima kuwa na BIMA ukiwa na biashara) MALIPO YA SERIKALI VAT /INCOME TAX Hujumuishwa katika hesabu ya kutoa Zakaah GHARAMA ZA KUUTOA MZIGO Ni sehemu ya matumizi MISHAHARA Ni sehemu ya matumizi USAFIRISHAJI Ni sehemu ya matumizi MADENI (MNAYODAI) Ikiwa yanatarajiwa kulipwa MADENI (MNAYODAIWA) Hamna uwezo wa kuyatolea FAIDA (Profit) Ni sehemu ya mali Na Allaah Anajua Zaidi