Zaaka ya fitri

17335

 

Maana ya zaka za fitri

Zaka ya fitri

Zaka aliyoifaradhisha Mtume (s.a.w)wakati wa kufungua katika kumalizika kwa mwezi wa Ramadhan.

Na imeitwa Zaka ya fitri kwasababu inawajibika pale mtu anapofungua kwa kumalizika mwezi wa Ramadhani.

Hukumu ya Zaka ya Fitri

Zaka ya Fitri ni lazima kwa kila Muislamu anayemiliki siku ya Idi na usiku wake pishi ya chakula cha ziada ya chakula chake cha siku na cha familia yake (nayo ni karibia kilo mbili na nusu).

Na yamlazimu mwenye kutoa Zaka ajitole Zaka nafsi yake, na mke wake, na wale ambao ni jukumu lake kuwalisha, hata mtoto alioko kwenye tumbo la mamake. Na dalili ya kuwajibika kwake ni ilivyopokewa kutoka kwa Ibn Umar radhi za Mwenyezi Mungu zimfikie asema: (Amefaradhisha Mtume (s.a.w) Zaka ya Fitri Pishi moja ya tende, au Pishi moja ya Shayir (aina ya nafaka) kwa mtumwa na muungwana, na mume na mke, na mdogo na mkubwa katika waislamu, na akaamrisha itolewe kabla ya watu hawajatoka kwenda kuswali (Idd) [Imepokewa na bukhari na muslim.].

Tende
Ngano

Wakati wa kutolewa Zaka ya Fitri

Wakati bora wa kutoa zaka za fitri ni kutoa siku ya idd baada ya kutokeza kwa alfajiri na kabla ya swala ya Idd na yaruhusiwa kutanguliza kuitoa kwa siku moja au siku mbili kabla siku ya Idd; kwa utkelazaji wa maswahaba. Wala haifai kuichelewesha hadi baada ya swala ya Idd; kwa Hadith ya Ibn Umar iliyotangulia: “Na akatuamrisha tuitoe kabla ya watu kutoka kuswali (Iddi)” Na katika Hadith ya Ibn Abbas t: “Atakayeitoa kabla ya swala basi ni Zaka inayokubaliwa, na atakayeitoa baada ya swala basi ni sadaka miongoni mwa sadaka” [Imepokelewa na abi daud.].

Kiwango cha kutolewa Zaka ya Fitri

Pishi moja [ Pishi ni sawa na kilo mbili na gramu arubaini (2.040 grms).]. kwa kila mtu, na kiwe ni chakula cha binadamu (kula) kama mchele, na tende, na ngano, kwa Hadith ya Abu Saii’d Alkhudhry radhi za Mwenyezi Mungu zimfikie asema: (Ilikuwa tunatoa katika wakati wa Mtume (s.a.w) siku ya Fitri pishi moja ya chakula”. Na akasema: “Na kilikuwa chakula chetu ni Shayir (aina ya nafaka), na zabibu, na aqitwu (Maziwa yaliyokaushwa) [ Aqtw: Maziwa yaliyokaushwa.]. na tende) [ Imepokewa na Bukhari]..

Na pishi ni sawa na 3.25kg kulingana na dhehebu la hanafia, ama jumhuri ya wanavyoni ni sawa na 2.040kg.

Na hukadiriwa vile vile kwa kujaza mkono mara nne kwa mwanamume wasitani

Wanaostahiki kupewa Zaka ya Fitri.

Inatolewa Zaka ya Fitri kwa yale makundi manane ambayo kwamba yanapewa Zaka, kwa maana (Zaka ya Fitri) ipo ndani ya kauli ya Mwenyezi Mungu: {Sadaka hupewa (watu hawa) – Mafakiri} (At-Tawbah: 60).

Hekima ya kutoa Zaka ya Fitri.

1. Kumsafisha aliyefunga kutokana na mambo ya upuzi na uchafu, kama ilivyopokewa kutoka kwa Ibn Abbas asema: (Amefaradhisha Mtume (s.a.w) Zaka ya Fitri kwa aliyefunga ili kumsafisha kutokana na upuzi na uchafu [ Arrafarh Uchafu: Maneno yanayosemwa ovyo.]., na ni chakula cha masikini) [Imepokewa na Abu Daud.].

Na hii ni kwamba aliyefunga mara nyingi haepukani na michezo, na maneno ya upuzi, na mambo yasiyo na faida katika maneno, basi ikawa hii Zaka inamsafisha aliyefunga kwa aliyoyafanya katika matamshi haya yaliyoharamishwa, au yaliyochukizwa kufanywa, ambayo kwamba yanapunguza thawabu za matendo, na kuharibu saumu.

2. Masikini na mafakiri kupata nafasi nzuri ya kimahitaji siku ya Idd ili kuepukana na kuomba ambako kuna udhalilifu na unyonge siku ya Idd, jambo hili (Zaka fitri) litawafanya wawe na furaha na bashasha, ili washirikiane na watu wengine katika kufurahia Idd.