Zaaka hukumu yake na masharti yake

24932

 

Maana ya zaka

Zaka kilugha.

Ni kukua kwa kitu na kuzidi.

Zaka kisheria.

Ni kiwango maalumu cha mali kinachotolewa wakati maalumu ili kupewa watu maalumu.

Umuhimu wa zaka

Zaka ni faradhi katika faradhi za Dini ya Kislamu, na ni nguzo ya tatu katika nguzo za Uislamu, Anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu: {Na simamisheni swala na toeni zaka} (Suratu An-Nur: 56),

Na akasema Mtume (saw): (Umejengwa Uislamu kwa mambo matano: Kushuhudia ya kwamba hapana mola apasaye kuabudiwa kwa haki isipokuwa Mwenyezi Mungu na kwamba Muhammad ni mja wake na ni Mtume wake, na kusimamisha Swala (tano za kila siku), na kutoa Zaka, na kuhiji nyumba tukufu (Al-ka’abah – ilioko Makkah), na kufunga Mwezi wa Ramadhani) [Imepokewa na Bukhari na Muslim.].

Hukumu ya anayekataa kutoa Zaka.

Anayekataa kutoa Zaka, ima amekataa kwa kupinga kwamba sio lazima kutoa [Juhuud: Ni kukataa kuwajibishwa kwake.], au kwa ubakhili.

1. Mwenye kukataa kutoa Zaka kwa kupinga.

Anayepinga wajibu wa Zaka basi amekufuru kwa makubaliano ya umma wote – ikiwa mtu huyu anajua vizuri wajibu wa Zaka; kwa sababu atakuwa amemzulia uwongo Mwenyezi Mungu na Mtume wake.

2. Anayekataa kutoa Zaka kwa ubakhili.

Atakayekataa kutoa Zaka kwa ubakhili wake basi huchukuliwa kutoka kwake Zakaa kwa nguvu na wala hawi kafiri kwa kufanya hivyo kukataa kutowa Zaka kwa ubakhili.

Na atakuwa ametenda dhambi kubwa miongoni mwa madhambi makubwa na ni uovu mkubwa sana.

Kwa kauli ya Mtume (saw) kuhusu wanaokataa kutoa Zaka: “Mtu yeyote aliye na hazina ya dhahabu na fedha na wala haitolei Zaka basi atachomwa nayo katika moto wa Jahannam na itajaaliwa kama vinoo ambavyo atapigwa navyo kwenye migongo na vipaji kila akipata ubaridi (yakipoa makali ya moto) anaregelewa tena (kupigwa navyo), mpaka Allaah Amalize kuhukumu waja wake siku ambayo ni sawa na miaka elfu khamsini. Kisha ndio ataoneshwa njia yake ikiwa ni ya peponi au motoni” [ Imepokewa na Bukhari.]

Na lau atapigana na kukataa kutekeleza amri ya zaka basi mpigeni vita mpaka arudi katika kutekeleza amri ya Mwenyezi Mungu, na atoe zaka, kwa kauli ya Mwenyezi Mungu U: {Lakini wakitubu na wakasimamisha swala na wakatoa zaka, basi iacheni njia yao (waacheni} (Suratu At-tawbah: 5).

Na kwa kauli ya Mtume (saw): (Nimeamrishwa niwapige watu vita mpaka washuhudiye ya kwamba hapana mola apasaye kuabudiwa kwa haki isipokuwa Mwenyezi Mungu na kwamba Muhammad ni Mtume wa Mwenyezi Mungu, na wasimamishe Swala, na watoe Zaka, watakapofanya hivyo basi imeharamishwa kwangu damu yao na mali yao isipokuwa kwa haki ya Uislamu, na malipo yao yako kwa Mwenyezi Mungu) [Imepokewa na Muslim.].

Na Abubakar t alipiga vita mtu yoyote ambaye alipinga wajibu wa zaka, na akasema: (Naapa kwa Mungu ya kwamba nitampiga vita yoyote aliyetenganisha kati ya Swala na Zaka, kwa hakika hiyo Zaka ni haki ya mali, Wallaahi kama wakinizuilia hata kwa (kamba ya) kutiwa shemere (anayofungwa mnyama kwenye pua zake) nitapambana nao madamu walikuwa wakiitoa kwa Mtume) [ Imepokewa na Bukhari.].

Hekima ya watu kuwajibika kutoa Zaka.

1. Ni kuzisafisha nafsi na kuzitakasa kutokana na ubakhili, na madhambi, na makosa, Anasema Mwenyezi Mungu U: “Chukua sadaka(zaka) katika mali zao, na uwaombee (dua) safishe na kwatakasa kwa ajili ya hizo (sadaka zao)” (suratu At-Tawbah: 103).

2. Kusafisha mali na kuikuza, na kutia baraka ndani yake, kwa kauli ya Mtume (saw): “Sadaka haipunguzi chochote (inapotolewa) katika mali” [Imepokewa na Muslim.].

3. Ni mja kupewa mtihani katika kutekeleza maamrisho ya Mwenyezi Mungu, na katika kutanguliza mapenzi yake kwa Mungu zaidi kuliko mapenzi yake ya kupenda mali.

4. Kuwaliwaza mafakiri na kuziba pengo la mahitaji ya wenye haja, jambo ambalo linaongeza mapenzi, na linatimiliza kiwango cha juu sana katika usaidizi wa kijamii baina ya waislamu wa eneo moja.

5. Kujizoezesha katika kutoa kwa njia ya Mwenyezi Mungu.

Fadhla ya kutoa Zaka

1. Ni sababu ya kupata Rehema za Mwenyezi Mungu, Anasema Mwenyezi Mungu U: {Na rehema yangu inaweza kukienea kila kitu. Lakini nitawaandikia (kweli kweli kabisa) wale wanaojikinga na yale niliyowakataza, na wanaotoa Zaka na wanaoziamini Aya zetu} (Al-A’raf: 156).

2. Ni sharti ya kupatikana Nusra ya Mwenyezi Mungu, Anasema Mwenyezi Mungu U: {Na bila shaka Mwenyezi Mungu humsaidia yule anayesaidia dini yake.Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu na Mwenye kushinda. Wale ambao tukiwamakinisha, (tukiwaweka uzuri) katika ardhi husimamisha Swala na wakatoa Zaka} (Al-hajj 40-41).

3. Ni sababu ya kufutiwa madhambi, Amesema Mtume (saw): (Na sadaka hufuta madhambi kama vile maji yanavyozima moto” [Imepokewa na Tirmidhi.].

Mali Yanayo wajibika jutolewa Zaka

1-(vitu) vinavyotoka ndani ya ardhi

2-Zaka za Dhahabu na Fedha

3-Zaka ya Mali ya biashara

4-wanyama wa mifugo


Masharti ya mtu kulazimika kutoa Zaka

1. Uislamu

Haikubaliwi Zaka kwa kafiri, kwasababu Mwenyezi Mungu U hakubali matendo yake.

2. Kuwa huru (muungwana).

Haikubaliwi kwa mtumwa kutoa Zaka, kwasababu mali yake ni milki ya bwana wake.

3. Kumiliki Nisabu.(kiwangu)

Maana ya Nisabu.

Nisabu.

Ni kiwango maalumu cha mali ambacho kwamba kikifikiwa basi inalazimika mali hayo kutolewa Zaka.

Masharti ya Nisabu.

1. Iwe Nisabu ni ziada ya mahitaji ya dharura ambayo kwamba mtu hatosheki kwa kuyapata mahitaji hayo, kama chakula, mavazi na makazi, kwasababu Zaka ni wajibu kwa lengo la kuwaliwaza mafukara. Hivyo basi inatakiwa mwenye kutoa hiyo mali asiwe ni mtu muhitaji.

2. Iwe Nisabu inamilikiwa na mtu maalumu umiliki wa kiukamilifu, basi haiwajibiki Zaka kwa mali ambayo haimilikiwi na mtu maalumu, kwa mfano: mali iliyokusanywa kwa lengo la kujenga msikiti, au mali iliyowekwa wakfu kwa maslahi ya ummah, au mali iliyoko kwenye hazina za jumuia za mambo ya kheri.

4. Mali kupitiwa na Mwaka

Mwaka

Ni mwaka wa kiislamu) uliyokamilika.

Na hii ni kwamba ipite miezi kumi na mbili ya kalenda ya mtizamo wa mwezi hali ya kuwa Nisabu iko kwenye miliki ya mwenye mali. Na sharti hili ni peke yake kwa pesa (dhahabu na fedha), na mapato ya biashara, na wanyama wa mifugo. Ama mazao ya kilimo na matunda, na madini, hazina iliyozikwa ardhini sio sharti kwa vitu hivi kupitiwa na mwaka.