Viungo Vipi Vinne Vya Mwanamke Vilivyokusudiwa Kwenye Jimai Ni Vipi, Na Kwa Nini Ni Hivyo Tu?

SWALI: Asslaam aleykum, Kheri za Allaah Subhaanahu wa taala ziwe juu yenu na sisi kwa kutusaidia kuijua dini yetu zaidi. JazaakumuAllaahu khair. Amepokea Abu Hurayrah (r.a.) kutoka kwa Mtume (s.a.w.w) kuwa amesema: “Anapokaa mmoja wenu baina ya viungo vinne vya mwili wake (yaani mkewe) na akafanya juhudi (jimai), basi inakuwa wajibu kuoga” (Ahmad na Muslim). Ni zipi sehemu nne zenyewe za mwanamke zilizo kusudiwa? Kwa nini zikawa ni hizo na si nyengine zozote? Natanguliza shukrani.

JIBU: Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho. Kwanza kabla hatujajibu swali lako, tunakukumbusha kuwa unapoandika jina la Allaah au Mtume, au Maswahaba usifupishe mbele yake kwa kuweka (S.W.) au (S.A.W.) au (R.A) kama ilivyozoelekea na wengi, bali andika kwa kirefu maneno hayo bila ya kuyafupisha. Andika (Subhaanahu wa Ta’ala) baada ya kumtaja Allaah, na andika Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) au (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) baada ya kumtaja Mtume. Hivyo ndivyo inavyopaswa, na ndio heshima zaidi na utukufu na ndivyo inavyotamkwa na si kama inavyofupishwa na wengi kimazoea. Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu viungo vinne vya mwanamke. Hadiyth hiyo ni sahihi na viungo vilivyokusudiwa ni miguu miwili na mikono miwili pia. Hivyo ndivyo viungo vilivyokusudiwa na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Ama kwa nini vikawa ni viungo hivyo si vyengine, Allaah Aliyetukuka ndiye Anayejua zaidi. Hata hivyo, kutajwa na wanachuoni kuwa hivyo ndivyo viungo vilivyokusudiwa ni kuwa aghlabu mwanamme huwa yuko juu ya mkewe wakati wa jimai, mwili wake huwa uko baina ya miguu yake na mikono ya mke ndio yenye kumshika ili kupata raha zaidi. Ilhali mume anakuwa juu ya viungo vyengine kama matumbo, kifua na kadhalika na sio baina yake. Na Allaah Anajua zaidi




Vitambulisho: