JIBU: Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho. Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu kufunga baada ya hedhi. Uislamu unatufahamisha kuwa mwanamke aliyebaleghe hafai kufunga ikiwa yuko katika hedhi au damu ya nifasi. Ikiwa kama ulivyosema ada yako ya mwezi inakuwa ni siku saba, na siku ya nane unajitwahirisha basi ukitaka kufunga unafanya yafuatayo: 1. Ikiwa ni funga ya faradhi inatakiwa uiweke kabla ya Alfajiri. Hivyo, ukiamka utakuwa katika funga utaoga ili uswali Swalah ya Alfajiri lakini ikiwa umechelewa kwa sababu moja au nyingine utaoga na kuendelea na funga yako. 2. Ama ikiwa ni funga ya Sunnah unaweza kuweka Niyah hata asubuhi baada ya Alfajiri. Ikiwa umechelewa kujitwahirisha funga yako itakuwa ni sahihi japokuwa utahitajika kuoga. Hata hivyo, unatakiwa uoge kabla ya Alfajiri uweze kuswali Swalah hiyo ya asubuhi. Kwa hivyo, funga yako katika hali zote mbili itakuwa ni sawa. Na Allaah Anajua zaidi