JIBU: Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho. Tunashukuru dada yetu kuhusu swali lako jingine la kutaka ufafanuzi kuhusu jibu tulilotoa kwako katika mas-ala ya kumlipia funga mama yako aliyeaga dunia. Awali ya yote ni muhimu tufahamu kuwa katika kulipa deni ikiwa ni lako au unamlipia mama mzazi tuwe ni wenye kufanya hima kulipa kabla Ramadhaan nyingine haijafika. Ikiwa utakuwa umepitia vyema jibu letu la mwanzo suala hili halingekuwa limejitokeza kwani limo ndani. Kwa ufupi ni kuwa nyinyi kama watoto wa aliyefariki mnatakiwa mumlipie mama yenu zile siku za Ramadhaan ambazo hakuweza kuzifunga. Ikiwa ni mwezi mzima mnafaa mfunge mwezi. Ikiwa mtamtolea na sadaka juu ya funga (yaani mkamfungia na kumtolea sadaka) itakuwa kheri zaidi kwa mama yenu. Allaah Aliyetukuka Anasema: “Na atakayefanya wema kwa radhi ya nafsi yake, basi ni bora kwake. na huku kufunga ni bora kwenu ikiwa mnajua” [2: 184]. Tunatumai tutakuwa tumeeleweka vizuri kuhusu hilo. Na Allaah Anajua zaidi