JIBU: Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho. Shukrani zetu za dhati kwa swali lako. Ni hakika kuwa haya mas-ala tumeyatia u’aswabiyah (kasumba) na ushabiki mpaka tukasahau Uislamu ambao umekuja kuondoa ujahiliya wa kikasumba na kitaifa. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Si katika sisi anayeita watu katika utaifa (kasumba n.k.) …” [Abuu Daawuud]. Sisi tunasema ipo misimamo miwili mikuu iliyochukuliwa na Wanachuoni wa Kiislamu – msimamo wa kufuata mwandamo wa kitaifa na kimataifa. Hata hivyo msimamo wa mwandamo wa kimataifa ndio wenye dalili za nguvu zaidi lakini hatuwachukulii wenye kufuata mwezi wa kitaifa kuwa funga zao ni batili. Hakika ni kuwa mwenye kujua usawa halisi wa funga na 'Ibaadah nyingine ni Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) peke Yake. Kisha huu msimamo wa kitaifa unakuaje? Kwa mfano, ikiwa mwezi umeonekana Namanga, Kenya na haukuonekana Namanga ya Tanzania au sehemu nyingine yoyote katika Tanzania, je Waislamu wa Tanzania watafunga? Ikiwa kweli watafunga kama inavyofanyika, kweli watakuwa wamefuata mwezi wa kitaifa au kieneo? Na Allaah Anajua zaidi