JIBU: Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho. Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu utohara wa nguo. Ni jambo linalofahamika kuwa yapo masharti ya kukubaliwa Swalaah ya mmoja wetu na moja wapo ni usafi pamoja na utohara wa nguo Muislamu anazoswalia akiwa ni mwanamme au mwanamke. Allaah Aliyetukuka Anamuagiza Mtume Wake na hivyo kwa kumwambia na kutuambia: “Na nguo zako, zisafishe” (al-Muddaththir [74]: 4). Mbali na kuwa tohara wa nguo ni katika masharti ya kukubaliwa Swalaah, pia Muislamu kila wakati anatakiwa yeye kuwa mswafi pamoja na nguo zake kuwa hivyo. Katika vitu viwili ambavyo umevitaja ni muhimu kwetu kuvielewa pamoja na hukmu yake, navyo ni manii na madhii. Vitu hivi viwili vina hukmu tofauti katika sheria. Manii si najisi lakini yakimtoka mwanamme au mwanamke ima kwa kuota au kwa kujamiiana au kwa sababu nyengine yoyote ile hatoweza kuswali mpaka aoge josho la janaba. Ilhali madhii ni najisi lakini huhitajii kuoga yanapokutoka kwa ajili ya kufikiria ngono au kwa sababu nyengine yoyote ile. Jambo ambalo linafaa kufanywa ni kuosha ile sehemu katika suruali ya ndani au nguo nyengine yoyote kwa maji kisha ukaivaa kwa ajili ya Swalaah na ikiwa imekauka inatosha kwako kukwaruza sehemu hiyo kisha ukaswali ukiwa umeivaa. Wapo wengine huwa na wasiwasi tu hata baada ya kuiosha nguo hiyo anaona hawezi kuswali akiwa ameivaa lakini hilo linatakiwa lisiwe tatizo. Wasiwasi kawaida unatokana na shetani na Uislamu pamoja na sheria yake umekuja kututoa katika hali hiyo. Kwa hiyo, ukiwa kazini utafanya hivyo tulivyokueleza na baadaye ukaswali bila ya tatizo lolote. Bonyeza viungo vifuatavyo upate maelezo zaidi: Tofauti Baina Ya Manii Na Madhii Na Hukumu Zake Za Ghuslu 003 Aina Za Najisi Mwanamke Akitokwa Na Majimaji, Je, Aoge Janaba? 008 Nini Hukumu Ya Majimaji (utoko) Yanayotoka Kwenye Utupu Wa Mwanamke Na Kile Kiitwacho Unyevunyevu Wa Utupu Wa Mwanamke? 028 Yanayotengua Wudhuu - 3 Na Allaah Anajua zaidi.