JIBU: Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho. Shukrani zetu za dhati kwa dada yetu muuliza swali kuhusu mas-ala ya kutanguka kwa wudhuu baada ya kumgusa mkeo au kinyume chake. Katika suala hili zipo rai tatu kutoka kwa wanazuoni: Kumguza mkeo kunavunja wudhuu daima: Hii ni kauli ya Ibn Mas‘uud na Ibn ‘Umar na rai ya madhehebu ya ash-Shaafi‘iy na Ibn Hazm. Haivunji Wudhuu kabisa: Hii ni kauli ya Ibn ‘Abbaas, Twaawuus, Hasan al-Baswriy na ‘Atwaa’ na kuchaguliwa na Ibn Taymiyah na kufuatwa na dhehebu la Abu Haniyfah. Hii ndio kauli iliyo sahihi. Huvunja kwa Matamanio: Rai ya madhehebu ya Maalik na Ahmad. Wenye kauli ya kwanza wanatoa dalili ifuatayo: “Au mmewagusa wanawake, na hamkupata maji, basi tayamamuni vumbi lilio safi” (5: 6). Na imesihi kutoka kwa Ibn Mas‘uud na Ibn ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhuma): “Kugusa bila jimai” (Tafsiyr atw-Twabariy kwa Isnadi sahihi). Lakini ametofautiana nao Ibn ‘Abbaas (Radhiya Allaahu ‘anhuma) aliyesema: “Kugusa na kukutana: Jimai, lakini Allaah Anatumia istiari Anachotaka kwa Anachotaka” (atw-Twabariy na Ibn Abi Shaybah kwa Isnadi sahihi). Tukiitazama ayah yenyewe (5: 6) ni dalili ya wazi inayounga rai ya (b) kwani kauli Yake Aliyetukuka: “Osheni”, ni twahara kwa kutumia maji kwa sababu ya hadathi ndogo. Kisha Anasema: “Na mkiwa na janaba basi ogeni”, hii nayo ni twahara kwa kutumia maji kwa hadathi kubwa. Kisha Akasema: “Na mkiwa wagonjwa au mmo safarini, au mmoja wenu ametoka chooni au mmewagusa wanawake, na hamkupata maji, basi tayamamuni vumbi lilio safi”. Na kauli Yake: “Basi tayamamuni”, ni badala ya twahara mbili. Hivyo kauli Yake: “Au mmoja wenu ametoka chooni”, ni bayana kwa sababu ndogo. Na kauli Yake: “au mmewagusa wanawake”, inabaini sababu kubwa. Hivyo, neno la kistiari lililotumika hapa ‘lamasa’ lina maana ya jimai. Zipo Hadiyth nyingi zinazoonyesha kugusa hakuvunji wudhuu. Miongoni mwazo ni: Hadiyth ya mama wa waumini ‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anha) aliyesema: Nilimkosa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) usiku mmoja kitandani, nikamtafuta na mkono wangu ukashika matumbo ya miguu yake akiwa Msikitini…” (Muslim, at-Tirmidhiy na Abu Daawuud). Amesema tena mama wa waumini ‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anha): Nilikuwa nikilala baina ya mikono ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), miguu yangu ikiwa kwenye Qibla chake, akisujudu alikuwa ananigusa nami nakunja miguu yangu …” (al-Bukhaariy na Muslim). Hakuna tofauti kabisa kuwa haijapokewa kutoka kwake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuwa alivunjwa wudhuu kwa kugusa (Ibn Taymiyah, Majmuu‘ Fataawaa, Mj. 21, uk. 410). Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa anawabusu wakeze na kuwakumbatia kisha anakwenda kuswalisha bila kuchukua wudhuu. Kisha hebu tuitazame Aayah ifuatayo ambayo itatufungia suala hili: “Akasema: Nitampataje mwana hali mwanaadamu yeyote hajanigusa, wala mimi si kahaba?” (19: 20). Aayah hii inatueleza mazungumzo baina ya Maryam na Malaika aliyetumwa kumpatia bishara ya kuwa atapata mtoto. Tazama Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) Anatuambia lile neno alilotumia Maryam alipouliza: “Lam yamsasniy bashar”, ambayo inatafsiriwa: “Ilhali mwanaadamu yeyote hajanigusa”. Suala ni kuwa je, mwanamke akiguswa na mwanamume anapata mtoto? La, mwanamke hapati mtoto ila kwa kitendo cha jimai baina yao. Ufupi wa maneno ni kuwa mwanamume kumgusa mkewe hakutangui wudhuu kabisa ikiwa ni kwa matamanio au bila ya matamanio. Inaweza kusemwa kuwa akitawadha kwa kugusana kwa matamanio bila kitendo cha ndoa ni vizuri kwa ajili ya kuzima yale matamanio kama ilivyokuwa inapendezeka mtu kutawadha pindi anapoghadhibika ili azime ghadhabu zake. Hivyo ukipenda unaweza kuchukua wudhuu ingawa si lazima. Pia tunakusahihisha kuwa madhehebu ya Sunni na Ibadhi si sawasawa; tofauti ni kubwa sana za 'Aqiydah kama mbingu na ardhi. Soma makala zifuatazo ujue tofauti hizo. Tofauti Ya Ya Ahlus-Sunnah Na Ibaadhi Khawaarij Inafaa Kuswalishwa Na Ibaadhi Na Hali Wao Hawaswali Nyuma Yetu? Na Allaah Anajua zaidi