Swalah ya kupatwa Jua na kupatwa Mwezi

11986

 

Maana ya kupatwa jua na Mwezi

Kupatwa Jua

Kuondoka mwangaza wa jua au baadhi yake mchana

Kupatwa Mwezi

Kuondoka nuru ya mwezi au baadhi yake Usiku

Hekima ya Kupatwa Jua na kupatwa Mwezi

Jua na Mwezi ni alama mbili miongoni mwa alama za Mwenyezi Mungu, Anawatisha kwavyo waja wake mpaka warudi Kwake. Mtume ﷺ Alisema: (Hakika jua na mwezi havipatwi kwa kufa mtu wala kwa kuishi kwake, lakini hivyo ni alama mbili miongoni mwa alama za Mwenyezi Mungu, huwatishia kwavyo waja Wake, basi vinapopatwa kimbilieni kuswali). [ Imepokewa na Abu Daud.]

Hukumu ya Swalah ya kupatwa jua na ya kupatwa mwezi

Ni sunna iliyokokotezwa (iliyotiliwamkazo) kwa kauli ya Mtume ﷺ: (Hakika jua na mwezi ni alama mbili miongoni mwa alama za Mwenyezi mungu, havipatwi kwa kufa mtu wala kuhuika kwake. Basi mkiona hilo muombeni Mwenyezi Mungu. Mpige takbiri, mswali na mtoe sadaka) [Imepokewa na Bukhari na Muslim.].

Wakati wa Swalah ya kupatwa jua na kupatwa mwezi

- Wakati wa Swalah ni kuanzia kupatwa jua au mwezi mpaka kumalizika kwake.

- Na mwenye kuswali atatimiza swala yake hata kama kupatwa kwa jua au kwa mwezi kumemalizika. Na hatorudia Swala akiwa amemaliza kuswali na kupatwa kwa jua au kwa mwezi hakujamalizika, bali Waislamu wataendelea kuomba dua na kuleta istighfari.

Namna ya Swalah ya kupatwa Jua na kupatwa Mwezi

Amepokewa ‹Aisha t akisema: (Lilipatwa jua wakati wa Mtume wa Mwenyezi Mungu ﷺ na Mtume wa Mwenyezi Mungu ﷺ akawaswalisha watu. Akasimama na akakirefusha kisimamo. Kisha akarukuu na akairefusha rukuu. Kisha akainuka kusimama akakirefusha kisimamo lakini kikawa chini ya kisimamo cha kwanza. Kisha akarukuu na akairefusha rukuu lakini ikawa chini ya rukuu ya kwanza. Kisha akasujudu na akairefusha sijida. Kisha akafanya katika rakaa ya pili kama alivyofanya katika ya kwanza. Kisha akamaliza na hali jua lishaachwa. Hapo akawahutubia watu, akamhimidi Mwenyezi Mungu na akamsifu kisha akasema: ‘Jua na mwezi ni miongoni mwa alama za Mwenyewzi mungu. Havipatwi kwa kufa yoyote wala kuhuika kwake. Basi mkiona hilo, Muombeni Mwenyezi Mungu, mpige takbiri, mswali na mtoe sadaka’) [Imepokewa na Bukhari.].

Na kulingana na hayo, itokeapo kupatwa kwa jua au kupatwa kwa mwezi:

1. Kutaitwa kuswaliwa kwa kusema: SWALAATU JAAMI’A “Haya imesimama Swala ya jamaa”

2. Watu wakikusanyikana, imamu atawaswalisha rakaa mbili ndefu, atainua sauti kwa kisomo, asome katika rakaa ya kwanza Fatiha, kisha asome sura ndefu. Kisha atarukuu na airefushe hiyo rukuu. Kisha ainuke na aseme: SAMI’ALLAHU LIMAN HAMIDA (Mwenyezi Mungu Amemsikia Aliyemsifu. Mola wetu! Sifa njema ni zako). Kisha asome Fatiha na sura ndefu, lakini fupi kuliko ile ya mwanzo. Kisha arukuu na airefushe rukuu hiyo, lakini fupi kuliko ya kwanza. Kisha ainuke na huku yuwasema: SAMI’ALLAHU LIMAN HAMIDA (Mwenyezi Mungu Amemsikia Aliyemsifu. Mola wetu! Sifa njema ni zako) kisha atasujudu sijida mbili ndefu, na atakaa baina ya sijida mbili wala asirefushe kikao, kisha atasimama kutoka sijida ya pili kwa Takbiri na ataswali rakaa ya pili sawa na rakaa ya kwanza kwa kisimamo chake na rukuu zake na sijida zake lakini sio ndefu kama rakaa ya kwanza, kisha atakaa tashahud nakusoma attahiyatu kisha atatowa salamu

Sunna za Swalah ya kupatwa Jua na Mwezi

1. Iswaliwe kwa jamaa, na akiswali kila mmoja peke yake si makosa.

2. Iswaliwe msikitini, na si makosa kwa wanawake kutoka kwenda kuswali.

3. Kuirefusha Swala, kwa kisimamo, rukuu na sijida, isipokuwa iwapo jua limeachwa au mwezi basi hapo itatimizwa kwa kufupishwa.

4. Rakaa ya pili itakuwa fupi kulingana na ya kwanza, kwa kisimamo chake, rukuu yake na sijida yake.

5. Kutolewa mawaidha baada yake, na kuwakumbusha watu kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu, na kueleza hekima ya kupatwa mwezi na jua, na kuwahimiza watu kufanya mambo ya utwiifu na kuacha mambo mabaya.

6. kuomba dua kwa wingi, kunyenyekea, kuomba msamaha, kutoa sadaka na mengineyo miongoni mwa matendo mema, mpaka Mwenyezi Mungu Awaondolee watu yale waliyo nayo.

7. Inafaa kuinua mikono katika dua kwenye Swala ya kupatwa jua au mwezi, kwa hadithi ya Abdurrahman bin Samurah t aliyesema: (Nikamjia Mtume ﷺ na yeye amesimama katika Swala na huku ameinua mikono yake) [Imepokewa na Muslim.]

Maelekezo

1. Swala ya kupatwa jua au mwezi hailipwi iwapo kupatwa kwa jua au mwezi hakukujulikana isipokuwa baada ya kuachwa.

2. Kuwa elimu ya kisasa imejua sababu ya kupatwa Jua na mwezi haifuti kuwa viwili hivyo ni miongoni mwa alama za Mwenyezi Mungu. Basi Muislamu atakikana ajishughulishe kwa ibada na kunyenyekea kwa Mwenyezi Mungu, na sio ajishughulishe na kuangalia na kuchunguza kupatwa kwa mwezi au jua. Abu Bakrah t amepokewa akisema: (Lilipatwa jua wakati wa Mtume wa Mwenyezi Mungu ﷺ akatoka na huku anakokota kishali chake). Hii inaonyesha vile anavyoogopa ﷺ.

3. Kupata rakaa kunakuwa kwa kupata rukuu ya kwanza pamoja na imamu. Basi aliyekosa rukuu ya kwanza na akapata ya pili, rakaa huwa ameikosa, na atailipa kwa namna zake baada ya imamu kutowa Salamu.

4. Swala ya kupatwa jua au mwezi huswaliwa hata katika nyakati zilizokatazwa kuswaliwa.

5. Haitoshi kuthibiti Swala ya kupatwa mwezi au jua kwa habari, bali ni mpaka kupatwa kuonekane waziwazi.