Swala ya jamaa na Fadhla zake

20567

 

Hukumu ya Swala ya jamaa

Sheria imeamrisha Swala ya jamaa kwa wanaume wanaoweza na imemuonya mwenye kuiwacha. Na Mtume ﷺ alidhamiria kuwachoma wale wasioihudhuria. Alafu Mtume ﷺ hakumruhusu kipofu kuacha jamaa, na dalili ya hilo ni: ya

1. Neno lake Mwenyezi Mungu Aliyetukuka kuhusu Swalah ya Hofu: {Na ukiwa na wao na ukawasimamishia Swala, basi na lisimame jopo miongoni mwao..} (4: 102).

Mwenyezi Mungu Aliyetukuka hapa Ameamrisha kusimamisha jamaa katika hali ya hofu ya kivita na safari, basi katika hali ya amani na ukazi ni aula zaidi.

2. Hadithi iliyopokewa na Abu Hurarah t kwamba Mtume ﷺ alisema: (Swala nzito zaidi kwa wanafiki ni Swala ya Isha na Swala ya Alfajiri. Na lau wao walijua Yaliyomo kwenye Swala mbili hizo, wangaliziendea japo kwa kujikokota [ Habwan: kujikokota kwa kitako.]. Na mimi nilidhamiria kutoa amri Swala kukimiwa, kisha nimuamrishe mtu awaswalishe watu, kisha nitoke na watu wakiwa na matita ya kuni niwaendee wale watu wasiohudhuria Swala niwachomee nyumba zao kwa moto) [ Imepokewa na Bukhari na Muslim.].

Na Mtume ﷺ hadhamirii kuwachoma wale wasiohudhuria jamaa isipokuwa hiyo jamaa ni wajibu. Pia hawasifiwi wale wanaoacha kuhudhuria kwa unafiki, isipokuwa ni kwa uajibu wake.

3. Hadithii ya kipofu aliyemtaka ruhusa Mtume ﷺ aswali nyumbani kwake – na hana mtu wa kumuongoza njia-, na Mtume ﷺ akamwambia: (Je unasikia mwito wa Swala?) Akasema: ”Ndio”. Akasema: (Basi itikia) [Imepokewa na Muslim.].

4. Hadithi iliyothubutu kutoka kwa Ibnu Mas’ud t kwamba yeye alisema: (Mwenye kufurahika kukutana na Mwenyezi Mungu Kesho hali ya kuwa ni Muislamu, basi ajilazimishe na hizi Swala. Kwani zitatangwazwa. Kwa hakika Mwenyezi Mungu Amemfaradhia Nabii wenu ﷺ nyendo za uongofu, na hakika hizi Swala ni miongoni mwa nyendo za uongofu. Na lau nyinyi mkiswali kwenye nyumba zenu kama anavyoswali nyumbani kwake huyu asiyehudhuria mgaliacha mwendo wa Nabii wenu, na lau mnaacha mwendo wa Nabii wenu mgalipotea. Na hakuna mtu yoyote anayejitwahirisha vizuri Kisha akaukusudia msikiti mmoja kati ya hii misikiti isipokuwa Mwenyezi Mungu Atamuandikia, kwa kila hatua anayoipiga, jema moja, Anampandisha daraja moja na Anampomoshea dhambi moja. Hakika niliona vile tulivyokuwa hakuna anayeacha kuihudhuria jamaa isipokuwa mnafiki anayejulikana unafiki wake. Na alikuwa mtu akiletwa na huku ameshikiliwa baina ya watu wawili- yaani akijishikiliza na wao- mpaka akasimamishwa kwenye safu) [ Imepokewa na Muslim.].

Hekima ya Swalah ya jamaa na Fadhla zake

1. Kujuana kwa ndugu na wanaopendana kwa ajili ya Mwenyezi Mungu wao kwa wao na kutilia nguvu ushikano wa mapenzi baina yao, mambo ambayo imani haiwi isipokuwa kwa hayo. Kwani hakuna njia ya Imani wala ya Peponi isipokuwa kwa kupendana kwa ajili ya Mwenyezi Mungu Aliyetukuka.

2. Kuepukana mja na unafiki na Moto kwa aliyewahi takbiri ya kufungia Swala siku arubaini mfululizo, kwa hadithi aliyoipokea Anas kutoka kwa Mtume ﷺ: (Mwenye kuswali kwa ajili ya Mwenyezi Mungu siku arubaini kwa jamaa, akawa anawahi takbiri ya kwanza, ataandikiwa kuwa mbali na Moto na kuwa mbali na unafiki) [ Imepokewa na Tirmidhi.].

3. Kukusanyika waislamu walio huku na kule na kuzizoweza nyoyo zao kheri na utengefu.

4. Kushikamana Waislamu na kusaidiana kwao baina yao.

5. Kudhihirisha ibada za Dini na nguvu yake.

6. Kuziunganisha nyoyo za Waislamu, kwa kumfanya mweupe na mweusi, Mwarabu na asiyekuwa Mwarabu, mkuu na mdogo, tajiri na masikini, wote wakawa pamoja ndani ya msikiti mmoja, nyuma ya imamu mmoja na katika wakati mmoja, wote wanaekelea kibla kimoja na muelekeo mmoja.

7. kuwatia hasira maadui wa Mwenyezi Mungu. Kwa kuwa Waislamu bado wana nguvu iwapo wataendelea kutunza utekelezaji Swala misikitini.

8. Kufutiwa dhambi na kupandishwa daraja. Imepokewa na Abu Huraira t kwamba Mtume wa Mwenyezi Mungu ﷺ alisema: (Je si niwajulishe kitu kinacho sababisha kufutiwa dhambi na Mwenyezi Mungu na kupandishwa daraja? Wakasema: “Kwani? Tujulishe ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu” Akasema: “Nikueneza maji ya kutawadhia kwenye viungo, na kuwa na hatua nyingi za kwenda msikitini, na kungoja Swala baada ya Swala. Kwani huko ndiko kujitolea katika kusimamisha Dini) [ Imepokewa na Muslim.].

9. Swala ya jamaa ni bora kuliko Swala ya mwenye kuswali peke yake kwa daraja ishirini na saba. Ibnu ‘Umar t amepokewa kwamba Mtume wa Mwenyezi Mungu ﷺ alisema: (Swala ya jamaa ni bora kuliko Swalah ya mwenye kuswali peke yake kwa daraja ishirini na saba) [ Imepokewa na Bukhari.]