NAMNA YA SWALAH YA IJUMAA

59965

 

Hukumu ya Swalah ya Ijumaa

Swalah ya Ijumaa ni wajibu kwa kila Muislamu, aliyebaleghe, asiye na udhuru wa kuiacha.

Dalili ya hilo:

1. Neno la Aliyetukuka: {Enyi mlioamini! Kukinadiwa Swala kwa siku ya Ijumaa, endeni kwa haraka kwenye utajo wa Mwenyezi Mungu, na muache biashara} [62: 9].

2. Neno la Mtume ﷺ: ( Hawatoacha watu kuhudhuria Ijumaa, au Mwenyezi Mungu Atapiga mihuri juu ya nyoyo zao, kisha wawe ni miongoni wa walioghafilika) [Imepokewa na Muslim].

Wale ambao Ijumaa si lazima kwao

Swala ya Ijumaa haimlazimu mwanamke, mtoto mdogo, msafiri na mgonjwa ambaye atadhurika akiihudhuria, lakini inasihi kwa wote hao. Wakihudhuria pamoja na wengine itawatosheleza na wakitohudhuria, wataswali Adhuhuri.

Mwanamke
Mtoto mdogo
Mgonjwa
Msafiri

Ubora wa siku ya Ijumaa

Siku ya Ijumaa ni bora ya siku za wiki ambayo Mwenyezi Mungu Amewahusu nayo Waislamu baada ya umma wengine kuwapotea. Na zimekuja hadithi nyingi kuhusu ubora wake, miongoni mwazo:

1. Neno lake Mtume ﷺ: ( Siku bora iliyotokewa na jua ni siku ya Ijumaa. Katika siku hiyo aliumbwa Adam, na katika siku hiyo alitiwa Peponi, na katika siku hiyo alitolewa humo) [Imepokewa na Muslim].

2. Amepokewa Abu Huraira t akisema kwamba Nabii ﷺ alisema: (Mwenye kuoga siku ya Ijumaa, akaswali alichokadiriwa kuswali, kisha akakaa kimya mpaka imamu akamaliza hutuba yake, kisha akaswali pamoja naye, atasamehewa dhambi zilizo baina ya siku ile na Ijumaa nyingine na nyongeza ya siku tatu) [Imepokewa na Muslim].

3. Amepokewa Abu Huraira t akisema kwamba Mtume wa Mwenyezi Mungu ﷺ alikuwa akisema: (Swala tano, na Ijumaa mpaka Ijumaa, na Ramadhani mpaka Ramadhani vinafuta dhambi zilizo baina yake, iwapo mtu atajiepusha na dhambi kubwa) [Imepokewa na Muslim].

Masharti ya kusihi Swalah ya Ijumaa

1. Wakati: Ijumaa haisihi kabla ya kuingia wakati wake wala baada ya kutoka wakati wake kama ilivyo kwa Swala nyinginezo. Na wakati wake ni wakati wa Swala ya Adhuhuri.

2. Ihudhuriwe na kundi la watu: Kwani haisihi kwa mtu mmoja. Na uchache wa jamaa ya Ijumaa ni watu watatu.

3. Kuwa mkazi: nako ni kuwa mtu ni mkazi wa kijiji kilichojengwa kwa mawe na vinginevyo miongoni mwa vitu vya kawaida vinavyotumiwa katika ujenzi wa makao, kisichohamwa kipindi cha kaskazi wala kusi. Ama watu wanaokaa majangwani na mahemani wanaohama mara kwa mara, Ijumaa inaswihi kwao lakini haiwalazimu.

4. Itanguliwe na hutuba mbili: kwa kuwa Mtume ﷺ alidumu nazo hutuba hizo.

Wakati wa Ijumaa
Inaswaliwa kwa jamaa
Watu wa majangwani

Namna ya kuswali Swalah ya Ijumaa

Swala ya Ijumaa ni rakaa mbili na kisomo katika rakaa hizo husomwa kwa sauti.Na ni sunna kusoma katika rakaa ya kwanza- baada ya Fatiha- sura ya Al-Jum’ah, na katika rakaa ya pili – baada ya Fatiha- kusoma sura ya Al- Munaafiquun, au asome katika rakaa ya kwanza sura ya Al-A’laa na katika ya rakaa ya pili asome sura ya Al-Ghaashiah. [ Imepokewa na Muslim.].

Hutuba mbili

Hukumu ya hutuba mbili

Hutuba mbili ni wajibu, nazo ni mojawapo ya masharti ya kusihi Ijumaa. Na zitolewa kwa lugha ya Kiarabu, iwapo wengi wa waliohudhuria wanafahamu Kiarabu na waelewa maana yake kwa ujumla, ili kuhimiza kujifunza Kiarabu na kutoenda kinyume na uongofu wa Mtume ﷺ.

Na iwapo wengi waliohudhuria hawafahamu lugha ya Kiarabu, basi hapana makosa kuitoa kwa lugha nyiginezo, kwani la msingi katika hutuba ni kufundisha na kuongoza, si utoaji hutuba tu, lakini iwe pamoja na kuchunga uletaji aya za Qur›ani kwa lugha ya Kiarabu- ikimkinika- kisha kufasiri maana yake.

Vikamilisho vya hutuba

Hutuba ya Ijumaa haina nguzo, isipokuwa hutuba inakuwa kwa kile kinachoitwa hutuba kikawaida. Lakini miongoni mwa vitu vinavyoifanya hutuba ikamilike ni vifuatavyo:

1. Kumsifu Mwenyezi Mungu.

2. Kuleta shahada mbili.

3. Kumswalia Mtume wa Mwenyezi Mungu ﷺ.

4. Kuusia watu kumcha Mwenyezi Mungu.

5. Kusoma sehemu ya Qur›ani.

6. Kuwaidhia.

Sunna za hutuba mbili

1. Kuhutubu juu ya mimbari.

2. Kuwatolea watu salamu anapopanda mimbari.

3. Kupambanua baina ya hutuba mbili kwa mwanya mdogo.

4. Kuzifupisha hizo hutuba mbili.

5. Kuwaombea Waumini dua.

Yanayokatazwa katika Swalah ya Ijumaa

1. Ni haramu kusema na imamu yuwahutubu siku ya Ijumaa, kwa kauli yake Mtume ﷺ: (Ukimwambia mwenzako siku ya Ijumaa “Nyamaza” na imamu yuwahutubu, basi umecheza) [ Imepokewa na Bukhari.].

2. Ni karaha kuruka shingo za watu, isipokuwa awapo ni imamu au mtu awaruke watu kuenda kwenye mahali penye nafasi hawezi kuifikia isipokuwa kwa kufanya hivyo.

Kuipata Ijumaa

Ni juu ya Muislamu afanye haraka kwenda Ijumaa mapema. Akichelewa kuhudhuria Swala na akaiwahi rukuu katika rakaa ya pili pamoja na imamu ataitimiza Swala kama ya Ijumaa. Na akitoiwahi rakaa ya pili. Basi ataitimiza kama Adhuhuri. Hivyo hivyo, mwenye kupitwa na Swala ya Ijumaa kwa sababu ya kulala au nyingine, basi ataiswali adhuhuri – yaani, ataiswali rakaa nne-

Yanayo pendekezwa siku ya Ijumaa

1. Kusoma sura ya Al-Kahf siku ya Ijumaa, kwa kauli ya Mtume ﷺ: (Mwenye kusoma sura ya Al-Kahf siku ya Ijumaa atapata mwangaza wa nuru baina ya Ijumaa mbili) [ Imepokewa na Haakim.].

2. Kumswalia Mtume ﷺ kwa wingi. Alipokewa Abu Ms’ud al- Answari t kuwa Mtume ﷺ alisema: (Niswalieni kwa wingi siku ya Ijumaa, kwani hakuna yoyote atakayeniswalia isipokuwa nitaorodheshewa Swala yake) [Imepokewa na Haakim.].

Kuoga na kujipaka manukato, kwa kauli yake Mtume ﷺ: (Mtu yoyote anayeoga siku ya Ijumaa, akajitwahirisha anavyoweza kujitwahirisha, akajipaka mafuta aliyonayo, au akajitia manukato ya nyumbani kwake, kisha akatoka asitie uhasama baina ya wawili, kisha akaswali kile alichoandikiwa kuswali, kisha akanyamaza kimya imamu anaposema, basi huyo atasamehewa dhambi zilizo baina ya Ijumaa ile na Ijumaa nyingine) [Imepokewa na Bukhari.].

Maelezo kuhusu Ijumaa

1. Lililo sunna kuhusu mimbari iwe ni daraja tatu, kwa kumfuata Mtume ﷺ.

Minbari yenye daraja tatu

2. Si katika sunna kile kinachoitwa “suratul Jumu’ah” ambapo wenye kuswali wanakaa kumsikiliza msomaji kuwasomea baadhi ya aya za Qur’ani mpaka kuadhiniwa Swala ya ijumaa au kutoa nashidi na dhikri kwa pamoja kupitia vipazasauti.

3. Mwenye kuswali akihudhuria na imamu anahutubu, basi na aswali rakaa mbili fupi kabla hajakaa, kwa kauli ya Mtume ﷺ: (Anapokuja mmoja wenu Ijumaa, basi na aswali rakaa mbili na azifupishe) [Imepokewa Ibn khuzema.].

4. Mweye kuhutubu ataomba akitumia kidole chake cha shahada, na hatainua mikono yake wakati wa kuomba dua isipokuwa katika kuomba mvua au kuomba mvua ikome. Huswain bin Abdurrahman t alipokewa akisema: (Nilimuona Mtume wa Mwenyezi Mungu ﷺ na yeye yuwahutubu, akiomba akisema hivi- akiaashiria kwa kidole chake cha shahada-) [Imepokewa na Ahmad.].

Ataashiria kwa kidole chake

5. Swala ya Ijumaa haina sunna ya kabla yake, lakini inapendekezwa aswali sunna ya kawaida kabla ya adhana, kwa kuwa Mtume ﷺ alisema: (Mwenye kuoga siku ya Ijumaa akajitwahirisha kwa anachoweza cha kujitwahirisha kisha akajipaka mafuta yake au akajitia manukato ya nyumnbani kwake, kisha akatoka kwenda Ijumaa, asiwafarakanishe baina ya watu wawili, na akaswali kile alichojaaliwa kuswali, na akanyamaza kimya imamu alipotoka kuja kuhutubu, basi atasamehewa dhambi baina ya Ijumaa ile na wiki nyingine) [Imepokewa na Daarimi.].

6. Sunna ya baada ya Ijumaa inaswaliwa rakaa mbili kwa hadithi iliyopokewa na Ibnu ‘Umar t kuwa alisema: (Alikuwa Mtume wa Mwenyezi ungu ﷺ akiswali rakaa mbili baada ya Ijumaa nyumbani kwake) [Imepokewa na Jamaa.],

au nne, kwa neno la Mtume ﷺ: (Atakayekuwa ni mwenye kuswali miongoni mwenu baada ya ijumaa, aswali rakaa nne) [Imepokewa na Muslim].

na lililo bora ni aziswali nyumbani kwake.

7. Idi na Ijumaa zinapokusanyika, kwa kutoka shakani ni aswali Idi na Ijumaa. Na akiswali Idi ni lazima, kwa uchache, aswali Adhuhuri. Na inaruhusiwa kwa watu wanaokaa mbali, wakiswali Idi, wasirudi kuswali Ijumaa. Amepokewa Iyaas bin Ramlah al- Shaami akisema: (Nilimshuhudia Mu’awia akimuuliza Zaid bin Arqam: “Je uliwahi kushuhudia pamoja na Mtume wa Mwenyezi Mungu ﷺ Idi mbili pamoja? Akasema: “Ndio. Aliswali Idi mwanzo wa mchana, kisha akatoa ruhusa kuhusu Ijumaa, akasema: ‘Atakaye kukusanya, basi na akusanye) [Imepokewa na Ahmad.].

Ingia katika kiungo kifuatacho upate maelezo zaidi:
Hukmu Ya Anayeswali Ijumaa Pekee Na Kuacha Swalaah Zilizobaki