Sijida ya kusahau, kushukuru na kisomo

25085

 

Kwanza: Sijida ya sahau

Maelezo kuhusu sijida ya kusahau

Sijida ya sahau

Ni sijida mbili ambzo mwenye kuswali anasujudu ili kuungaunga kasoro iliyopatikana katika Swala yake kwa ajili ya kusahau.

Sababu za sijida ya kusahau

Sababu za kusujudu sijida ya kusahau ni tatu: kuwa na shaka, kuongeza na kupunguza.

1- Kufanya shaka

Kufanya shaka

Nako ni kuwa na shaka baina ya vitu viwili, ni kipi kilichotokea.

Kufanya shaka katika Swala kuna gawanyika mara mbili:

1. Kufanya shaka baada ya kuswali:

Shaka hii haishughulukiwi.

- Mfano wake: Mtu alifanya shaka baada ya kuswali Alfajiri, Ameiswali rakaa mbili au tatu? Shaka hii haishughulikiwi, mpaka awe na yakini, hapo atafanya kulingana na yakini yake.

2. Kufanya shaka akiwa ndani ya Swala:

Shaka hii ina hali mojawapo ya hali mbili:

a. Liwe na nguvu kwake yeye mojawapo ya mambo mawili:

Na hapa atafanya kile kilicho na nguvu kwake na atasujudu kwa kusahau baada Salamu.

Mfano wake: Mtu anaswali adhuhuri na akaifanyia shaka rakaa: je ni ya pili au ni ya tatu, lakini lililo na nguvu kwake ni kuwa ni ya tatu, hili litaifanya hiyo rakaa kuwa ni ya tatu na ataitimiza Swala yake, kisha atasujudu kwa kusahau baada ya Salamu.

Na dalili ya hilo ni kauli ya Mtume ﷺ: (Akifanya shaka mmoja wenu na ajitahidi kujuwa la sawa ni lipi, kisha atowe Salamu, kisha asujudu sijida mbili) [Imepokewa na Ibnu Hibbaan.].

Anatowa Salamu kisha Atasujudu sijida ya kusahau

b. Lisimdhihirikie katika mambo mawili, ni lipi lenye nguvu:

Huyu atajengea juu ya kichache, hivyo basi atatimiza Swala yake na atasujudu sijida ya kusahau kabla ya Salamu.

Mfano wake: Mtu anaswali Adhuhuru akaifanyia shaka ile rakaa anayoiswali: ni ya pili au ya tatu? Kusiwe na uzito wa jambo lolote kati ya haya mawili. Basi huyu atajengea juu ya uchache na ataihesabu kuwa ni ya pili, na atatimiza Swala yake na atasujudu sijida ya kusahau kabla ya Salamu.

Na dalili ya hilo ni kauli ya Mtume ﷺ: (Akifanya shaka mmoja wenu katika Swala yake, asijue ameswali ngapi, tatu au nne, basi aitupilie mbali shaka yake na ajengee juu ya yakini yake kisha asujudu sijida mbili kabla hajapiga Salamu) [Imepokewa na Muslim.].

Anatowa Salamu kisha Atasujudu sijida ya kusahau

2. Kuzidisha

Nako ni kule kuongeza Rukuu au Sijida kwa mwenye kuswali…

Na kuzidisha kuko namna mbili

a. Awe mwenye kuswali ataikumbuka pale wakati wa kuzidisha.

Na hapo itamlazimu aiache ile ziada na atimize Swala yake kisha asujudu sijida ya kusahau baada ya kupiga Salamu.

- Mfano wake: Mtu anaswali Adhuhuri, akasimama kuleta rakaa ya tano kisha akakumbuka katikati. Hapa itamlazimu akae haraka na atimize Swala, kisha asujudu sijida ya kusahau baada ya kupiga Salamu.

b. Awe mwenye kuswali akakumbuka baada ya kuifanya.

Huyu atatimiza Swala yake kisha atasujudu sijida ya kusahau baada ya kutowa Salamu. Na dalili yake ni hadithi ya Ibnu Mas›ud t kwamba Mtume ﷺ aliswali Adhuhuri rakaa tano. Akaambiwa: “Je Swala imeongezwa?” Akasema: “Kwani kuna nini?” akaambiwa: “Umeswali rakaa tano”, akasujudu sijida mbili baada ya kuwa ashatowa Salamu ) [Imepokewa na Bukhari.].

3. Kupunguza

Nako ni kupunguza mwenye kuswali nguzo au wajibu miongoni mwa nguzo au wajibu za Swala.

1. Kupunguza nguzo

Iwapo nguzo hiyo ni takbiri ya kufungia Swala, basi Swala inabatilika, kwa kuwa itakuwa haikufungika tangu mwanzo. Na iwapo nguzo hiyo si takbiri ya kufungia Swala, basi hapo pana mojawapo ya hali mbili:

a. Ni aikumbuke mwenye kuswali baada ya kufikia mahali pa hiyo nguzo kwenye rakaa ifuatayo:

Hii inafuta ile rakaa ambayo nguzo hii iliachwa na inasimamisha rakaa ifuatayo mahali pake.

- Mfano wake: Mtu aliyesahau kurukuu katika rakaa ya kwanza, kisha akakumbuka naye yuko kwenye rukuu ya rakaa ya pili kuwa alisahau kurukuu kwenye rakaa ya kwanza.Mtu huyu ataizingatia rakaa ile kuwa ni rakaa ya kwanza na hataizingatia ile rakaa iliyotangulia, na atakamilisha Swala yake, kisha atasujudu kwa kusahau baada ya kutowa Salamu.

Anatowa Salamu kisha Atasujudu sijida ya kusahau

b. Aikumbuke mwenye kuswali kabla hajafikia mahali pa nguzo hiyo kwenye rakaa ifuatayo:

Hapa itamlazimu airudie ile nguzo iliyoachwa ailete na zile za baada yake, na ataikamilisha Swala yake, kisha atasujudu kwa kusahau baada ya Salamu.

- Mfano wake: Mtu alisahau sijida ya pili na kikao cha kabla yake katika rakaa ya kwanza, akakumbuka hilo baada kuinuka kutoka kwenye rukuu katika rakaa ya pili. Yeye atarudi kukaa na kusujudu, kisha ataikamilisha Swala yake, kisha atasujudu kwa kusahau baada ya Salamu.

2. Kupunguza jambo la wajibu:

Akisahau mwenye kuswali jambo moja la wajibu miongoni mwa mambo ya Swala ya wajibu basi hapo pana hali tatu tu:

a. Aikumbuke kabla hajaondoka pale mahali pa wajibu huo katika Swalah.

Na hapa ataileta huo wajubu na hatolazimika na jambo lolote.

b. Aikumbuke baada ya kuondoka pale mahali pa nguzo hiyo katika Swala kabla hajafika kwenye nguzo ifuatayo.

Na hapa atarudi aifanye nguzo hiyo na asujudu sijida ya kusahau baada ya kutoa Salamu.

c. Aikumbuke baada ya kufikia kwenye nguzo inayoifuatia.

Na hapa ataendelea na Swala yake na hatairudia na atasujudu kwa kusahau kabla ya kutoa Salamu.

Mfano wake: mtu aliinuka kutoka kwenye sijida ya pili ya rakaa ya pili ili ainuke kwenda kwenye rakaa ya tatu hali ya kusahau kikao cha Atahiyatu ya kwanza. Kisha akakumbuka kabla ya kusimama kuwa yeye amesahau kikao cha Atahiyatu. Basi huyu atajituliza akae kwa kikao cha Atahiyatu, kisha ataikamilisha Swala yake, na hatolazimiwa na jambo lolote.

Akiwa atakumbuka baada ya kuinuka na kabla ya kulingana sawa katika kusimama, atarudi akae na asome Atahiyatu, kisha akamilishe Swala yake, na asujudu kwa kusahau kabla ya kutoa Salamu.

Akikumbuka baada ya kulingana katika kusimama, kikao cha Atahiyatu hakimlazimu na kwa hivyo hatakirudia, atakamilisha Swala yake na atasujudu sijida ya kusahau kabla ya kutoa Salamu.

Na dalili ya hilo ni hadithi ya Abdullah bin Buhainah t kwamba Mtume ﷺ aliwaswalisha Adhuhuri akainuka katika rakaa mbili za kwanza bila ya kukaa, na watu wakainuka pamoja naye. Hata alipomaliza kuswali na watu wakamngojea kupiga Salamu, alipiga takbiri na hali yeye amekaa, akasujudu sijida mbili kabla ya kutoa Salamu, kisha akatoa Salamu) [Imepokewa na Bukhari].

Kwa yaliyotangulia inabainika kwetu sisi kwamba sijida ya kusahau inakuwa kabla ya kutoa Salamu na pia baada ya kutoa Salamu.

Namna ya kusujudu sijda ya kusahau

Sijida ya kusahau ni kama sijida ya Swala, atapiga takbiri wakati wa kusujudu, na wakati wa kuinuka kutoka kwenye sijida, na atasema yale yanayo semwa katika sijida na kati ya sijida mbili.

Maelezo

1- Akipiga Salamu mwenye kuswali kabla ya Swala kukamilika na asikumbuke isipokuwa baada ya kipindi kirefu, basi atairudia Swala upya, na akikumbuka baada ya kipindi kifupi kama dakika mbili tatu, ataikamilisha Swala yake na atasujudu kwa kusahau baada ya Swala.

2- Inamlazimu maamuma kumfuata imamu katika sijida ya kusahau hata kama alimfuata baada kusahau.

3- Ikikusanyika kwa mwenye kuswli sahau mbili, mahali pa mojawapo ni kabla ya Salamu na mahali pa pili ni baada ya Salamu, basi yeye atasujudu sijida ya kusahau mara moja kabla ya kuleta Salamu.

Takbiri ya kufungia Swala
Atasujudu sijida ya kusahau

Pili: Sijida ya kushukuru

Sijida ya kushukuru

Ni kusujudu kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kupata neema au jambo la furaha au kuepukwa na jambo kuchukiza na mfano wake.

Na dalili ya kuwa Sijida ya kushukuru imewekwa na Sheria ni hadithi iliyopokewa na Abu Bakrah t kwamba Mtume ﷺ alikuwa likimjia jambo la furaha au akabashiriwa nalo hupomoka hali ya kusujudu kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu [Imepokewa na Abuu Daud.].

Namna ya sijida ya kushukuru

Ataleta takbiri hali ya kusujudu na aseme SUBHANA RABBIYAL A’ALAA (Kutakasika ni kwa Mola wangu Aliye juu kabisa) na amsifu Mwenyezi Mungu na amshukuru kwa neema Alizompa yeye, kisha ainuke kutoka kwenye sijida yake na asilete takbiri wala asipige Salamu.

Tatu: Sijida ya kisomo

Sijida ya kisomo

Ni sijida ambayo mwenye kusoma husujudu anapofika kwenye aya yenye Sijida.

Dalili ya kuwa Sijida ya kisomo imewekwa na Sheria ni hadithi iliyothubutu kutoka kwa Ibnu ‹Umar t kuwa alisema: (Mtume alikuwa akitusomea sura yenye sijida na yeye akasujudu na sisi tukasujudu) [ Imepokewa na Bukhari.].

Kusujudu kunakuwa pale mwenye kusoma anapopita kwenye aya yenye sijida ndani ya Swala, iwe ni ya siri au ya dhahiri, au nje ya Swala. Na sijida yenyewe haishurutiswi kuwa na udhu.

Namna ya kusujudu kwa kisomo

- Mwenye kusoma au kusikiliza Qur›ani atapiga takbiri kwa ajili ya kusujudu na aseme: (Kutakasika ni kwa Mola wangu Aliye juu kabisa), na aombe kwa kusema: (Uso wangu umemsujudia Yule Aliyeuumba, akapasua masikizi yake na maoni yake kwa uwezo Wake na nguvu Zake) [ Imepokewa na Tirmidhi.].

(Ewe Mola! niandikie kwa sijida hii malipo yaliyoko Kwako, na uniondolee kwayo dhambi, uijaalie ni akiba yangu kwako wewe, na uikubali kutoka kwangu mimi kama ulivyoikubali kutoka kwa mja wako Daud) [ Imepokewa na Tirmidhi.].

- Kisha apige takbiri na ainuke kutoka kwenye sijida, akiwa yuko katika Swala, na akiwa hayuko katika Swala, atainuka bila takbiri wala Salamu.

Aya zinazokusanya sijida za kisomo

AL-A’raaf Aya (206) Al-Furqaan Aya (60)
Ar-Raa’d A ya (15) An-Naml Aya (25)
An-Nah’l Aya (49) Assajda Aya (15)
Al-Israa Aya (107) S’aad Aya (24)
Maryam Aya (58) Fuss’ilat Aya (37)
Al- Hajj Aya (18) Annajm Aya (62)
Al- Hajj Aya (77) Al-Inshiqaaq
Al-A’laq

Maelezo

1- Msafiri juu ya kipando akisoma aya ya Sijida, atashuka kwenye kipando chake na asujudu kwa kisomo. Likitomsahilikia hilo ataashiria kwa kichwa chake kusujudu.

2- Msomaji akiirudia aya ya sijida, inamtosheleza yeye kusujudu mara moja.

3. Si makosa kusujudu kwa ajili ya kisomo katika nyakati ambazo zimekatazwa kuswaliwa.

4- Iwapo msomaji hakusujudu, basi msikilizaji hatasujudu kwa kuwa yeye ni mfuasi wake na ni mwenye kumfuata katika kisomo.

5- Mwenye kumsikia msomaji bila kukusudia kumsikiliza, kama akiwa ni mpita njia au ameshughulika na jambo lingine, basi hatamfuata kwenye kusujudu kwa kuwa hakuwa akimfuata katika kisomo.