swaumu za Sunna

43460

 

 

Maana ya saumu za swaumu

swaumu za Sunna

Saumu yoyote amabayo sio ya lazima na mtu anaifunga ili kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu mungu

Na saumu ya sunna ina fadhila kubwa na malipo makubwa. Katika Hadithi Al-Qudsy kutoka kwa Abu Hureirah t Anasema: Amesema Mtume (saw): “Kila kitendo chema cha mwanadamu malipo yake huongezwa, jema moja hulipwa kwa kumi mfano wake mpaka kufikia mara sabini. Anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu: Isipokuwa saumu, kwani hiyo ni yangu mimi, na mimi ndiye mwenye kuilipa” [Imepokewa na Bukhari na Muslim.].

Siku ambazo kwamba ni sunna kufunga.

1. Siku sita katika mwezi wa Shawwaal (Mfungo mosi)

Kwa kauli ya Mtume (saw): (Atakayefunga Ramadhani, kisha akafuatiliza kwa kufunga siku sita za Shawwaal, itakuwa ni kama aliyefunga mwaka mzima) [Imepokewa na Muslim.].

Sawasawa awe amezifunga siku sita hizi kwa pamoja kufuatana au siku mbalimbali zisizofuatana.

2. Kufunga Siku Tisa za Mwanzo wa Mwezi wa Dhulhijjah. (Mfungo tatu)

Kwa kauli ya Mtume (saw): (Hakuna masiku ambayo matendo mema ni bora zaidi mbele ya Mwenyezi Mungu kuliko masiku haya – yaani masiku kumi ya Dhulhijjah – wakasema (maswahaba): hata jihadi kwa njia ya Mwenyezi Mungu? Akema (Mtume): “Hata jihadi kwa njia ya Mwenyezi Mungu, isipokuwa mtu aliyetoka (kwenda jihadi) yeye mwenyewe na mali yake, wala asirudi na chochote (yaani akafa vitani)” [Imepokewa na Bukhari.].

Na masiku haya yakatiliwa nguvu zaidi na siku ya A’rafa kando na hajj – nayo ni siku ya tisa ya mwezi wa Dhulhijjah; kwa kauli ya Mtume (saw): (Kufunga siku ya A’rafa nataraji kwa Mwenyezi Mungu kusamehewa mtu madhambi ya mwaka kabla yake, na mwaka uliyo baada yake) [Imepokewa na Muslim.].

3. Kufunga siku ya A’shuura na siku iliyo kabla yake.

A’shuura

Ni siku ya kumi katika mwezi wa Muharam (Mfungo nne).

Kwa kauli ya Mtume (saw): (Na kufunga siku ya A’shuura nataraji kwa Mwenyezi Mungu kusamehewa kwa mtu madhambi ya mwaka uliyo kabla yake) [ Imepokewa na Muslim.].

Na sababu ya kufunga siku hii ni kama ilivyothibiti kutoka kwa Abdillahi ibn Abbas anasema: (Aliingia Madina Mtume (saw) akawaona Mayahudi wamefunga siku ya A’shuura, akasema Mtume: Ni nini hiki (mnachofanya)? Wakasema: Hii ni siku njema, siku hii ndiyo siku Mwenyezi Mungu aliyowaokoa wana israili kutokamana na maadui zao, basi akaifunga siku hii Nabii Musa. Akasema Mtume: Basi mimi nina haki zaidi kwa Musa kuliko nyinyi, akaifunga Mtume siku hiyo na akaamrisha watu kuifunga) [Imepokewa na Bukhari.].

Na inapendekezwa vile vile kufunga siku ya tisa, kwa ilivyo pokelewa kutoka kwa Mtume (saw) Alisema (Lau nitaishi mpaka Mwaka ujao nitafunga siku ya tisa) [ Imepokewa na Muslim.]

4. Kufunga Masiku meupe ya kila mwezi

Masiku meupe

Nayo ni tarehe kumi na tatu, na kumi na nne, na kumi na tano ya kila mwezi katika miezi ya kiislamu, na yameitwa meupe; kwasababu usiku wa masiku haya hunga’ra kwa mwangaza wa mwezi.

Kama ilivyothibiti kutoka kwa AbdulMalik ibn Minhal kutoka kwa babake: Kwamba (babake) alikuwa pamoja na Mtume (saw) akasema (kumwambia mwanaye – AbdulMalik): Alikuwa Mtume (saw) akiwaamrisha kufunga masiku meupe, na akisema: (Masiku) haya ni saumu za mwaka) [Imepokewa na Ibnu Hibbaan.]

5. kufunga siku mbili – jumatatu na alhamisi katika kila wiki.

Kama ilivyopokewa kutoka kwa Abu Hureira t kwamba Mtume ﷺ amesema: “Hupandishwa matendo (juu kwenda mbinguni) kila jumatatu na alhamisi, basi napenda matendo yangu yapandishwe hali ya kuwa nimefunga” [Imepokewa na Tirmidhi.].

6. Kufunga siku Moja na kula siku Nyingine

Bora katika funga za sunnah ni saumu ya Nabii Daud juu yake iwe amani – Alikuwa akifunga siku moja na kuacha siku moja; kutoka kwa Abdillahi ibn A’mru t Anasema: Amesema Mtume (saw): (Hakika saumu ya kupendeza sana mbele ya Mwenyezi Mungu ni saumu ya Daud, na alikuwa akifunga siku moja na kula siku moja) [Imepokewa na Nasaai.].

7. Kufunga Mwezi wa Muharam.

Kutoka kwa Abu Hureira t Anasema: Amesema Mtume (saw): (Saumu ilio bora baada ya Ramadhani ni saumu ya mwezi wa Muharam) [Imepokewa na Muslim.].

8. Kufunga Mwezi wa Shabani

Kutoka kwa Usama ibn Zaid t Asema: Nilisema: (Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, sijapata kukuona ukifunga mwezi wowote mfano wa unavyofunga Shabani. Akasema: Kwa sababu huo ndio mwezi ambao watu wanaghafilika kati ya Rajabu na Ramadhani, na ndio mwezi ambao matendo hupandishwa juu kwa Mola wa walimwengu, basi napenda matendo yangu yapandishwe hali ya kuwa nimefunga) [Imepokewa na Nasaai.].

Ama Katazo lililo kuja katika hadithi ya Mtume (saw) Inayo sema (Ifikapo nusu mwezi wa shabani Musifunge) [Imepokewa na Ibnu Khuzeymah.]

inachukuliwa ni kwa Yule anae khusisha nusu ya mwisho wa shabani kwa kufunga, au kutounganisha shabani na Ramadhani, ama Yule alifunga mwanzo wa shabani, wala asikhusishe mwisho wa shabani wala asiunganisha na ramadhani hapana ubaya kwa mtu huyu kufunga.

Masiku yanayo haramishwa kufunga na yanayo chukiza

Kwanza: Masiku yanayo haramishwa

1. Ni haramu kufunga siku za idd Mbili Amepokeya Abuu Hurayra t Kwamba Mtume (saw) (Amekataza kufunga siku mbili: Siku ya Adh’ha na Siku ya Fitr) [Imepokewa na Muslim.]

2. Ni haramu kufunga siku za Tashriiq, nazo nisiku tatu baada ya iddul’Adh’ha, Amesema Mtume (saw) (siku za tashriiq ni siku za kula na kunywa) [Imepokewa na Muslim.]

Lakini inafaa kwa mahujaji kufunga ikiwa hija yake ilikuwa ni kwania ya Tamattu na Qiran na asipate mnyama wa kuchinja kwa neno lake Mwenyezi Mungu (Basi mwenye kujistarehesha kwa kufanya umra kisha ndio akahiji, basi achinje mnyama aliye mwepesi kumpata.na asiye pata afunge siku tatu katika hija na siku saba mtakapo rudi) [Al-baqara: 196]

3. Niharamu kufunga Siku ya shaka, nayo nisiku ya thalathini ya mwezi wa Shabani, ikiwa usikuwake ni usiku wa mawingu au vumbi lakutowezekana kuonekana Mwezi, Kwa neno lake Ammaar t (Mwenye kufunga siku ya Shaka hakika amemuasi babake Qaasim (saw) [Imepokewa na Tirmidhi na akasema ni hadithi nzuri swahihi.]

Pili: Masiku Ambayo ni makruhu kufunga

1. Ni makuruhu kupwekesha mwezi wa Rajabu kwa kufunga, kwa sababu alama za watu wa jahiliya ni kutukuza mwezi wa Rajab, na katika kuhusisha kuufunga ni katika kuhuisha alama zao

2. Ni makuruhu kufunga siku ya ijumaa kwa kukatazwa kufanya hivyo, Amepokeya Abuu Hureyra t Amesema: Amesema Mtume (saw) ( Asifunge mmoja wenu siku ya ijumaa ila afunge siku kabla yake au siku baada yake) [ Imepokewa na Muslim.]

Isipokuwa ikisadifu ada ya mtu basi atafunga wala si makuruhu kwake kufunga.

3. Ni Makruhu kuunganisha Saumu, nao ni mtu kufunga siku mbili mfululizo bila ya kufunguwa, kwa sababu Mtume alikataza kuunganisha Saumu, Amepokeya Abdullah bin Umar t Amesema Amekataza Mtume (saw) Kuunganisha wakasema kumuuliza wewe waunganisha akasema (mimi si kama nyinyi mimi nalishwa na kunyeshwa) [Imepokewa na Bukhari na Muslim.]

Saumu kwa mtizamo wa ki-afya
Hakika ya saumu inasaidia katika kutibu magonjwa ya ngozi, na sababu ya hili ni kwamba saumu inapunguza kiwango cha maji ndani ya damu na kusababisha damu kupungua kiwango chake katika ngozi, ambapo jambo hili linapelekea kuongezeka kwa kinga za ngozi na kuweza kupambana dhidi ya viini hatari na magonjwa ya tumboni yanayosababishwa na bacteria.

Maelezo

1. Muislamu nilazima kujilazimisha katika Ibaada zake na sharia ya Mwenyezi Mungu, asifunge siku zilizo katazwa na sharia kufunga, au kujikhusishia masiku kufunga ambao sharia haikuhusisha kama kufunga siku ya ishirini na saba mwezi wa Rajab au kufunga Nusu Shabani, kwa kauli yake Mtume(saw) (Mwenye kuzusha katika dini yetu hii jambo ambalo halimo ataregeshewa mwenyewe) [ Imepokewa na Muslim.]

2. Muislamu ni lazima awe Mbali na kutukuza Alama za Makafiri, asihishimu Masiku wanayoyatukuza kwa kufunga au kwa Sampuli ya Ibaada aina yoyote ile.



Vitambulisho: