Nyudhuru/Ruhusa za mtu kula ndani ya mwezi wa Ramadhani

9681

 

 

Ruhusa za mtu kula ndani ya mwezi wa Ramadhani

1. Ugonjwa

Yaruhusiwa kwa mgonjwa kula ndani ya mwezi wa Ramadhani; kwa kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu: { Na atakaye kuwa mgonjwa katika nyinyi au katika safari (akafungua baadhi ya siku), basi (atimize) hisabu katika siku nyingine} (Al-Baqarah – Aya 184).

Na ugonjwa amabao waruhusiwa mtu kufungua ni ugonjwa unaosababisha dhiki kwa mgonjwa akifunga, au unaleta madhara kwa mgonjwa iwapo atafunga.

- Kula kwa mgonjwa

Atakapokula mgonjwa (ndani ya Ramadhani) - na ugonjwa wenyewe ni wenye kutarajiwa kupona – inamlazimu kulipa siku alizokula pindi atakapopona; kwa kauli ya Mwenyezi Mungu U: {….basi atimize hisabu katika siku nyingine} (Al-Baqarah –Aya 184).

Na ikiwa ugonjwa ni usiotarajiwa kupona – kama vile ugonjwa wa kudumu au ni mtu mzee sana asiyeweza kufunga kabisa, itabidi mtu kama huyu alishe kila siku maskini mmoja nusu kibaba cha mchele au mfano wake katika chakula kinachotumika eneo lake.

2. Safari

Inaruhusiwa kwa msafiri kula ndani ya Mwezi wa Ramadhani, na inamlazimu kuilipa saumu hiyo baadaye, kwa kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu: {Na atakayekuwa mgonjwa katika nyinyi au katika safari (akafungua baadhi ya siku), basi atimize hisabu katika siku nyingine} (Al-Baqarah –Aya 184).

Na safari inyoruhusiwa mtu kula ni ile ambayo kwamba mtu anaruhusiwa kufupisha swala, na ni ile safari ambayo ki-ada ya kwao inatambulika kuwa safari, kwa sharti iwe safari yenyewe inaruhusika kisheria, ikiwa ni safari ya maasi (iliyo kinyume na sheria), au safari ya malengo ya ujanja wa kutaka kufungua basi hairuhusiwi katika safari hiyo kufungua.

Na iwapo msafiri atafunga basi saumu yake inakubalika na atalipwa ujira, kwa hadithi ya Anas ibn Malik asema: “Tulikuwa tukisafiri pamoja na Mtume (saw) wala hakumkosoa aliyefunga kwa asiyefunga, wala ambaye hakufunga kwa aliyefunga” [Imepokewa na Bukhari.].

Lakini kwa sharti ya kwamba saumu hii isimpe shida katika safari yake, ikiwa itampa shida, au itamletea madhara, basi kula kwa msafiri kama huyu ni bora zaidi, kwasababu Mtume (saw) alimuona katika safari mtu aliyefunga amekuwa tabaani sana kwa joto jinsi lilivyokuwa kali, na watu wamemzunguka, akasema Mtume (saw): “ Si katika wema kufunga safarini “ [Imepokewa na Bukhari.].

3. Mimba na kunyonyesha

Mjamzito au mwenye kunyonyesha akiwa atakhofia nafsi yake kudhurika kwa kufunga basi anaruhusiwa kula, na atailipa saumu hiyo kama vile mgonjwa; kwa kauli ya Mtume (saw): “Hakika ya Mwenyezi Mungu amemuondoshea msafiri kufunga, na akamshurutisha kuswali, na akamuondoshea (akampa ruhusa ya kula) mjamzito na mwenye kunyonyesha saumu) [Imepokewa na Tirmidhi.].

Na iwapo atakhofia juu ya mtoto wake peke yake bila ya kukhofia nafsi yake anaweza kula, na akailipa baadaye, na anatakiwa alishe kila siku (atakayokula) maskini mmoja; kwa kauli ya Ibn Abbas: t (Na mwenye kunyonyesha na mjamzito watakapokhofia juu ya watoto wao wanaweza kula, na walishe maskini mmoja) [Imepokewa na Abuu Daud.].

4. Damu ya Heidhi na Nifasi

Mwanamke mwenye hedhi au nifasi ndani ya Ramadhani analazimika kula, na ni haramu kwake kufunga, na lau atafunga saumu yake haikubaliwi, na itamlazimu kuilipa tena saumu hiyo, kama ilivyothibiti kutoka kwa A’isha alipoulizwa kulipa kwa mwenye hedhi saumu bila ya kulipa swala – akasema: (Ilikuwa tukitokwa na damu ya hedhi, na tulikuwa tukiamrishwa kulipa saumu, wala hatukuamrishwa kulipa swala) [Imwpokewa na Bukharin a Muslim.]

Kulipa swaumu

- Muislamu akila siku moja katika Mwezi wa Ramadhani bila ya dharura ni lazima atubie kwa Mwenyezi Mungu na aombe msamaha, kwa sababu kula bila ya sababu ni katika Madhambi makubwa, na ni lazima kulipa masiku aliyokula baada ya Ramadhani kwa haraka, na hii na kwa kauli ya wanachuoni, kwa sababu alikuwa haruhusiwi kula, na asili ni kutekeleza kwa wakati wake.

- Mtu anapokula kwa dharura kama vile mwanamke akiwa katika hedhi, au nifasi, au kwa ajili ya ugonjwa au safari au dharura nyingine aliyo ruhusiwa na sharia basi nilazima kulipa masiku aliyo kula baada ya Ramadhani, ila akishindwa kufunga, na silazima kulipa kwa haraka bali anaruhusiwa kuchelewesha kwa sharti asiingiliwe na Ramadhani nyingine, kwa hadithi iliyopokelewa na bibi Aisha t Amesema (Nilikuwa na daiwa saumu ya ramadhani na nisiweze kuilipa ila mwezi wa shabani kwa kumshughulikia Mtume wa Mwenyezi Mungu(saw)[Imwpokewa na Bukharin a Muslim.] Lakini inapendekezwa kufanya haraka kukidhi saumu kwa sababu ni kujitoa kwenye dhima, na ni uzuri kwa mtu asije likamtokezea jambo asiweze kufunga baadae kama ugonjwa na mfano wake.

- Na mtu akichelewa kukidhi saumu kwa dharura mpaka akaingiliwa na ramadhani nyingine basi atalazimika kufunga baada ya Ramadhani ya pili.na hana kafara.

- Na akichelewesha kukidhi bila ya dharura yoyote ile mpaka akaingiliwa na Ramadhani ya pili, basi ni juu yake kwa kauli ya jamhuri ya wanafiqihi, alipe saumu pamoja na kulisha masikini kila siku aliyo kula nusu ya pishi ya chakula cha watu wa mjini.

- Haisharutishwi katika kulipa saumu kufuatanisha, bali inasihi kufuatanisha na kufunga siku mbali mbali kwa neno lake Mwenyezi Mungu “Na atakayekuwa mgonjwa katika nyinyi au katika safari (akafungua baadhi ya siku), basi atimize hisabu katika siku nyingine” (Al-Baqarah –Aya 184).

- Na mwenyezi Mungu hakushurutisha kufuatanisha, na kama ingekuwa ni lazima Mwenyezi mungu angelibainisha.

- Na mtu akiwa anadaiwa na saumu ya Ramadhani, mwanzo atalipa deni la saumu kabla ya kufunga saumu ya sunna kwa sababu Faradhi ndio Asili na ndio inayo tangulizwa, lakini lau atafunga sunna kabla ya kukidhi inafaa, hasa ikiwa saumu yenyewe ina fadhila na asipo funga atakosa fadhila hizo kama siku kumi za fungo nne na saumu ya siku ya arafa na siku sita za mwezi wa mfungo mosi (shawwal) kwa sababu wakati wa kulipa ni mrefu, ingawa Ubora ni alipe kwanza.

- Mwenye kuacha kulipa saumu mpaka akafa, ikiwa alikwa na dharura kwa kutolipa kwake basi hana lolote, kwa sababu hakukusudia, ama kama alikuwa hana dharura yoyote, basi atalishwa masikini kwa ajili yake, ikiwa ni saumu ya Ramadhani, ama ikiwa anadaiwa saumu ya Nadhiri atamfungia yeye walii wake, na baadhi ya wanachuoni wamesema Mtu anapokufa na akawa na deni la saumu basi atamfungia yeye walii wake sawa iwe ni deni la Ramadhani au Nadhiri kwa hadithi ya bibi Aisha t kwamba Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw)Amesema (Mwenye kufariki na Akawa anadaiwa Saumu basi atamfungia yeye walii wake) [ Imwpokewa na Bukharin a Muslim.]

- Na kwa hadithi ya Ibnu Abbas t Asema alikuja mtu kwa Mtume (saw)akasema ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu mama yangu amefariki na anadaiwa saumu ni mlipie? Akasema (Ndio: deni la Mwenyezi Mungu lina haki zaidi kulipwa) [Imwpokewa na Bukharin a Muslim.]



Vitambulisho: