JIBU: Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho. Ama kuhusu hiyo Swalaah inayojulikana kama Swalaatul-Awwaabiyn, Swalaah hiyo kwa jina lingine ni Swalaah ya Adhw-Dhwuhaa. Swalaah hiyo ambayo ni ya Adhw-Dhwuhaa, inaweza kuswaliwa kwa rakaa mbili, nne, sita au nane. Huswaliwa baada ya jua kuchomoza hadi mpaka kabla ya wakati wa Adhuhuri. Inapendezewa kuichelewesha Swalaah hiyo hadi wakati jua limekuwa kali, na dalili ni Hadiyth ifuatayo: Kutoka kwa Zayd bin Arqam (Radhwiya Allaahu ‘anhu), ambaye amesema: Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alienda kwa watu wa Qubaa na akawakuta wanaswali. Akasema: “Swalaatul-Awwaabiyn ni ile (inayoswaliwa) pindi ngamia wadogo wananyanyua miguu yao (kwa joto kali la mchanga).” [Muslim] Kwenye riwaya nyingine kutoka kwa Imaam Ahmad (Rahimahu Allaah) kutoka kwa Zayd bin Arqam (Radhwiya Allaahu ‘anhu), kwamba Nabiy ((Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuja au aliingia kwenye Msikiti wa Qubaa baada ya jua kupanda, akakuta watu wanaswali. Akasema: “Swalaatudhw-Dhwuhaa inapaswa kuswaliwa wakati ngamia wadogo wananyanyua miguu yao (kwa joto la mchanga).” Imaam An-Nawawiy (Rahimahu Allaah) amesema: “Tamko au jina ‘Swalaatul-Awwaabiyn’ ni wakati ngamia wadogo wanaponyanyua miguu yao (kwa joto la mchanga), inaashiria wakati mchanga umekuwa hauvumiliki kwa joto la jua lililopiga mchana huo, na mchanga huchoma nyayo za ngamia hao wadogo hadi kushindwa kuvumulia na kuwabidi kunyanyua miguu yao kila mara kukwepa ukali wa joto hilo la mchanga. ‘Al-Awwaab’ maana yake ni yule mtiifu, au yule mwenye kuelekea kwenye utiifu. Hadiyth vilevile inaashiria au kuelekeza wakati bora wa kuiswali Swalaah hiyo, japo inaruhusika kuiswali wakati wowote baada ya jua kuchomoza hadi kufikia wakati wa jua liko utosini nyakati za kabla ya Adhuhuri.” [Sharh Muslim Lil-Nawawiy] Na ama kuhusu rakaa sita za Swalaah baada ya Maghrib, hilo limepokelewa kutokana na Hadiyth dhaifu bali ni Munkar kwa mujibu wa Wanachuoni wa Hadiyth. Rakaa zilizothibiti baada ya Swalaah ya Maghrib ni mbili tu. Kuhusu hiyo Hadiyth ya fadhila za kuswali rakaa sita baada ya Maghrib, imepokelewa na At-Tirmidhiy, Ibn Maajah, na imesimuliwa na Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) amesema, Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Yeyote atakayeswali rakaa sita baada ya Maghrib na hakusema chochote kibaya baina ya hizo (rakaa), atapata ujira sawa na kufanya ‘ibaadah ya miaka kumi na mbili.” Imaam At-Tirmidhiy (Rahimahu Allaah) ameeleza kuwa alimsikia Muhammad bin Ismaa’iyl (Imaam Al-Bukhaariy) akisema kuwa ‘Umar bin ‘Abdillaah bin Abiy Khath’am ambaye yumo katika wasimulizi wa Hadiyth hiyo juu, ni Munkar Al-Hadiyth, na akasema ni dhaifu sana. Kadhaalika, Imaam Al-Albaaniy (Rahimahu Allaah) amesema katika kitabu ‘Dhwa’iyf At-Tirmidhiy’ kuwa Hadiyth hiyo ni dhaifu sana. Vilevile ziko Ahaadiyth kama hiyo ambazo zinashaji’isha (zinahimiza) kuswali baina ya Maghrib na ‘Ishaa, lakini zote ni dhaifu. Kama tulivyotangulia awali huko juu kueleza, rakaa mbili baada ya Maghrib ndizo zilizthibiti. Nazo zinajulikana kama ‘Raatibah’ au ‘Swalaah za Rawaatib’ Nazo zimetajwa katika Hadiyth ifuatayo: Mama wa Waumini Ummu Habiybah Ramlah bint Abiy Sufyaan (Radhwiya Allaahu ‘anhaa) anasimuliwa kuwa alimsikia Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): “Nyumba itajengwa Peponi kwa kila Muislamu anayetekeleza rakaa kumi na mbili za kujitolea zisizokuwa za lazima (Fardh) mchana na usiku, kwa kutafuta radhi za Allaah.” [Muslim] Rakaa hizo za kujitolea zisizo za fardhi kwa mujibu wa Imaam An-Nasaaiy na Imaam At-Tirmidhiy ni hizi zifuatazo: 2 kabla ya Swalaah ya Alfajiri. 4 kabla ya Swalaah ya Adhuhuri. 2 baada ya Swalaah ya Adhuhuri 2 baada ya Swalaah ya Maghrib. 2 baada ya Swalaah ya ‘Ishaa. Na Allaah ni Mjuzi zaidi.