Mwenye Deni La Swawm Ikiwa Ana Ugonjwa Wa Kuhitaji Kutumia Dawa Kwa Wakati Bila Kuacha, Afanyeje?

SWALI: Assalam alaikum Ndugu zangu waislamu. Niko na swali kuhusu kulipa deni la swaumu. Mdogo wangu alikuwa mgonjwa muda mrefu myaka kama miwili ilo pitaga alikuwa hawezi kufunga lakini mwaka jana yaani 2006 kwa uwezo wake Allah alipata matibabu akajaliwa kufunga na badae akapata uja uzito sasa baada ya kujifungua ikaingiya mwezi mtukufu wa Ramadhani yaani mwaka jana sasa 2007 hakujaliwa kufunga, Sasa kabla hata hajanza kulipa deni lake hilo akaumwa kwenda hospitali wamemwambiya kuwa ule ugonjwa wake umerudi tena sasa inambidi kurudi kutumiya dawa tena kwa haraka na dawa zenyewe ina mbidi kunywa vidonge vi ine (4) asubuhi na vingine (4), sasa swali lake ni hili anaweza akafanya aje kusema hili deni lake lilipwe kwa ajili hivi hospitali wamemwambiya vidonge hivyo asi miss hata siku moja kunywa. Ndugu zangu waislamu ninawaomba jibu Allah njo atakaye walipa kwa kazi mnayo ifanya ila kwa mimi ninawaombeya pepo ya Firdaus INSHA ALLAH. Nina maliziya hapa nakuwatakiyeni kila lakheri Allah awaepushe na shari za dunia. Ni Dada yenu katika Imaan

JIBU: Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho. Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu kulipa deni la Swawm kwa dada yako ambaye ni mgonjwa. Ama kuhusu suala hilo Allaah Aliyetukuka Ametubainishia kwa uwazi kabisa pale Aliposema: “Na atakayekuwa mgonjwa katika nyinyi au katika safari (akafungua baadhi ya siku), basi atimize hesabu katika siku nyingine. Na wale wasioweza, watoe fidia ka kumlisha masikini. Na atakayefanya wema kwa radhi yake, basi ni bora kwake” (Al-Baqarah [2]: 184). Kwa hakika Aayah hiyo iliyo juu iko wazi kabisa, nayo ni kuwa Muislamu akiwa ni mgonjwa wakati wa Ramadhaan, ugonjwa unaotarajiwa kupona atalipa siku alizoacha baada ya Ramadhaan. Na lau ugonjwa wake hautarajiwi kupona kabisa basi atamlisha masikini kwa kila siku aliyoacha katika siku za Ramadhaan bila kufunga. Na kwa huyu dada yako tunavyoona kuwa anatarajiwa kuwa atapona wala msikate tamaa, kwani alikuwa na ugonjwa huo huo naye akapona. Jaribuni matibabu na Allaah Atampa shifaa ya haraka. Kitu ambacho mnatakiwa kufanya ni kuweza kumpata daktari Muislamu ambaye ana ghera na Uislamu wake ili awape ushauri ulio mzuri na mwema. Kwa kuwa wapo Waislamu wenye ugonjwa ya kutumia vidonge, na wao bila wasiwasi hutumia vidonge hivyo baada ya kufungua Swawm wakati wa Magharibi na vidonge vingine kabla ya Alfajiri ya kweli wakati wa daku (au suhuri). Hata hivyo, yote hayo yafanywe bila ya taklifu ndio tukakushauri upate ushauri wa daktari mahiri lakini Muislamu mzuri pia. Kwa muhtasari ni kuwa, ikiwa mgonjwa hatarajiwi kupona atalisha masikini mmoja kwa kila siku asiyofunga huyo dada yenu. Na ikiwa anatarajiwa kupona kama awali basi atafunga anapopona. Na ikiwa anaweza kumeza vidonge kwa mpango basi anaweza kufunga na kumeza vidonge bila shida yoyote. Bonyeza viungo vifuatavyo upate maelezo zaidi: Hakuweza Kufunga Kwa Muda Wa Miaka Minne Kwa Sababu Ya Ugonjwa Kulipa Swawm Na Kafara Tunamuomba Allaah Aliyetukuka Ampe shifaa dada yenu kwa ugonjwa alio nao. Na Allaah Anajua zaidi




Vitambulisho: