JIBU: Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho. Rai za Maulamaa kuhusu kumuingilia mwanamke anapomaliza hedhi kabla ya kufanya ghuslu zimepatikana nazo ni kama zifuatazo: Rai ya kwanza ni kwamba hadi mwanamke amalize hedhi na afanye ghuslu (aoge josho). Hii kutokana na kauli ya Allaah: “Na wanakuuliza juu ya hedhi. Waambie, huo ni uchafu. Basi jitengeni na wanawake wakati wa hedhi. Wala msiwaingilie mpaka watwaharike. Wakishatwaharika basi waendeeni Alivyokuamrisheni Allaah. Hakika Allaah Huwapenda wanaotubu na huwapenda wanaojisafisha” [Al-Baqarah: 222]. Rai ya pili ni kwamba mwanamke anapomaliza hedhi mumewe anaweza kumuuingilia pindi yakifanyika matatu yafuatayo; Atakapokuwa ametwaharika kutokana na damu ya hedhi yote na kutoka kwake kumesimama kabisa, hapo anaruhusiwa kurudia kitendo cha jimai baada ya kuosha sehemu inayotoka damu, akafanya wudhuu au akakoga josho kamili (Ghuslu). Vyovyote kati ya haya matatu atakavyofanya itaruhusiwa kwao kurudia kitendo cha jimai kutokana na kauli ya Allaah: "…Humo wamo watu wanaopenda kujitakasa. Na Allaah Anawapenda wanaojitakasa" (At-Tawbah 9:108) Lakini rai ilyo na nguvu kabisa ni rai ya kwanza kwamba mwanamke ajitwaharishe kwa maana afanye ghuslu (aoge josho) ndipo mumewe aweze kurudia kitendo cha jimai. Kwa maelezo zaidi ingia katika kiungo kiufatacho: Je, Inafaa Kumuingilia Mke Baada Hedhi Lakini Kabla Ya Ghuslu? Na Allaah Anajua zaidi