JIBU: Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho. Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu mwasho wa kawaida ambao mwanamke anapata. Mwasho kama huo kawaida unawapata si wanawake pekee bali hata wanaume. Kwa hiyo, awali ya yote tungetoa nasaha kwa dada yetu akaenda kwa daktari ili ajue ni kitu gani kwani unaweza au anaweza kukaa hivyo na huo ugonjwa alio nao ukawa unazidi. Tukija sasa katika swali lako tunasema hivi: Mwanamke ni tofauti na mwanamme kwa kuwa katika sehemu za mbele za siri za mwanamke kunakuwa na majimaji ambayo hayadhuru nayo ni tofauti na manii. Kwa hiyo, mwanamke mwenyewe anaweza kuelewa wakati ametokwa na manii na wakati anapokuwa na majimaji ya kawaida. Kuhusu manii Ummu Salamah (Radhiya Allaahu ‘anha) amesema: Alikuja Ummu Sulaym (Radhiya Allaahu ‘anha) – mke wa Abu Twalhah (Radhiya Allaahu ‘anhu) – kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: “Ewe Mtume wa Allaah! Hakika Allaah Haoni haya juu ya ukweli. Je, mwanamke anahitajia kuoga anapoota?” Akaseme Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): “Ndio, anapoona maji?” (Al-Bukhaariy na Muslim). Hivyo, mwanamke anapoona manii katika nguo yake inakuwa wajibu wake kuoga na ikiwa hakuona basi hakuna kuoga hata akikumbuka kuwa aliota. Hii ni kwa mujibu wa Hadiyth ya mama wa Waumini ‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anha) aliyesema: “Aliulizwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): kwa mtu anayeona unyevunyevu wala asikumbuke kuwa aliota?” Akasema: “Ataoga”. Na mtu aliyedhani kuwa ameota lakini asione unyevunyevu?” Akasema: “Hatooga” (Abu Daawuud na at-Tirmidhiy). Tanbihi: ü Mwanamke kwa yote ni kama mwanamme sawa kwa sawa, kumaanisha kuwa akitokwa na manii kwa kuota au kwa matamanio basi inabidi aoge josho la janaba. ü Mwenye kutokwa na manii bila shahwa (matamanio) kwa sababu ya ugonjwa, baridi na mfano wake, hapaswi kuoga kwa kauli yenye nguvu na sahihi nayo ni madh-hab ya jamhuri kinyume na kauli ya Imaam Shaafi‘iy na Ibn Hazm. Wamejumlisha wanazuoni uwajibu wa kuoga kwa kutokwa na manii kwa matamanio ukiwa macho na kwa kuota pamoja na kutokwa na manii. Kwa muhtasari, mwanamke hutokwa na majimaji aina nyingi, mfano majimaji ya kawaida, manii, madhii na wadii. Ni akitokwa na manii tu ndio atapaswa kuoga. Hivyo, hayo majimaji yanayotoka ni manii nayo katika kujikuna anaingiwa na matamanio, itabidi aoge na bila shaka atakuwa anajua tofauti baina ya majimaji na maji ya manii. Ingia katika viungo vifuatavyo upate maelezo zaidi: Tofauti Baina Ya Manii Na Madhii Na Hukumu Zake Za Ghuslu Hukmu Ya Wadii Na Madhii .Na Allaah Anajua zaidi
Ingia katika kiungo kifuatacho upate maelezo zaidi:
Ghuslu - Wakati Wa Mwisho Kukoga Janaba Katika Mwezi Wa Ramadhaan