JIBU: Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho. Shukran sana kwa ndugu zetu kuhusu swali hili la ndoa na mke kukimbia kutoka katika nyumba ya mumewe. Hili kwa hakika ni suali nyeti, na haiyumkiniki kulitatua tatizo hili kwa jibu fupi bila maelezo ya ziada lakini Insha'Allaah kwa taufiki ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) tutajaribu kuzitazama pande nyingi za suala hili. Mwanzo kuweza kutatua tatizo ni muhimu kujua ni kwa sababu gani mke alitoroka kutoka kwa mumewe. Je, mume hamtimizii mkewe mahitaji yake ya kisheria? Je, mume yu amdhulumu na kumyanyasa mkewe? Au ipo shida gani nyengine. Au mke ameamua tu kutoroka nyumba ya mumewe bila ya makosa yoyote kwa upande wa mume? Ikiwa makosa ni ya mume basi inabidi mume ajirudi na kujirekebisha ili wapate kuishi katika hali ambayo ni nzuri. Hapa mume anaweza kwenda kwa mke na wazazi wake ili wakae pamoja na wazazi wa mke pamoja na mke ili waweze kusuluhisha jambo hilo. Na ikiwa hawakusikilizana na kuwa hapana kheri ya wao kuwa pamoja basi ni bora mume kutoa talaka ili kumuacha huru mke aweze kuolewa na mume mwengine. Ikiwa mke ndiye aliyeasi na kutoka katika twaa ya mume bila makosa yoyote kutoka kwa mume basi hii kisheria inakuwa ni nashiza upande wa mke. Suluhu baina upande wa mke na mume inaweza kufanyika ili kutafuta maafikiano na kurudiana kwa wema. Lakini ikiwa mume ametaka arudi na mke akakataa basi huyo mke huwa bado hajaachika na hawezi kuolewa na mume mwengine mpaka mume amuache. Kwa wakati huo mume hatakuwa na jukumu aina yoyote ya kumlisha na kumpatia mahitaji yake mpaka mke atakaporudi katika twaa ya mumewe. Mke kama huyo ikiwa ndiye mkosa atakuwa ni mwenye kuchukiwa na Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala). Kuhusu swali la tatu, Swawm ya mke huyu itakuwa imefaa ila tu atakuwa vile vile katika makosa ya kutokukaa kwa mumewe katika Ramadhaan na madamu hakuachika bado, basi atakuwa hakutumiza haki za mume zinazompasa kutimiza na kesho siku ya Qiyaamah ataulizwa kuhusu jukumu lake hilo. Na Allaah Anajua zaidi