Miongoni mwa adabu za kuswali

7859

 

 

Swalah ni ibada kuu. Muislamu katika ibada hiyo anaelelekea kwa moyo wake na mwili wake kwa Mwenyezi Mungu Aliyetukuka. Hivyo basi inatakikana itanguliwe na matayarisho ya kiroho na ya kimwili, ili aingie katika swala akiwa hana kitu cha kumshughulisha na aitekeleze kwa njia sahihi, na kwa hivyo imewekewa mambo yafuatayo:

1. Ikhlasi (kumtakasia Mwenyezi Mungu)

Mwenyezi Mungu U Anasema: {Na hawakuamrishwa isipokuwa wamuabudu Mwenyezi mungu hali ya kumtakasia Yeye Dini, hali ya kuwa na msimamo thabiti, na wasimamishe Swala na watoe Zaka, na hiyo ndiyo Dini ya mila iliyolingana sawa} [Al-Bayinah: 5].

Na Mwenyezi Mungu hakubali amali njema yoyote isipokuwa ibada ya kutakasiwa Yeye, isiyokua na kujionyesha wala kutaka sifa wala aina yoyote ya kumshirikisha Mwenyezi Mungu.

2. Kueneza maji kwenye viungo vya kutawadha

Nako ni kutawadha vizuri kwa njia kamilifu.

Abu Huraira (RA) alipokewa akisema kwamba Mtume wa Mwenyezi Mungu ﷺ alisema: (Je, siwajulishi nyinyi kitu ambacho kwacho Mwenyezi Mungu hufuta dhambi na hupandisha daraja? Wakasema: “ kwani? Tujulishe, ewe Mtume wa Mwenyezi mungu!” Akasema: Ni kueneza maji kwenye viungo vile itakikanavyo katika kutawadha [ Al-makarih: ni vile vinavyomsumbua mtu kama baridi na mfano wake.] , kukithirisha hatua za kwenda misikitini, na kungojea Swala baada ya Swala, kwani huko ndiko kujifunga kwenye utiifu wa Mwenyezi Mungu [ Ribatw: Kujifunga nafsi juu ya utiifu wa Mwenyezi Mungu.]) [Imepokewa na Muslim.].

3.Kutoka mapema kwa ajili ya Swalah

Nako ni kutoka mapema ili kupata fadhila za kungojea Swala. Abu Huraira ﷺ amepokewa akisema kwamba Mtume wa Mwenyezi mungu ﷺ amsema: (Mmoja wenu huzingatiwa anaendelea kuwa kwenye Swala kwa mda ambao anasubiri swala) [ Imepokewa na Bukhari.].

4. Kumtaja Mwenyezi Mungu

- Amtaje Mwenyezi Mungu anapotoka nyumbani kwa kusema: (Kwa jina la Mwenyezi Mungu, nimetegemea kwa Mwenyezi Mungu, Hapana hila za kujiepusha na maasia wala nguvu za kufanya mambo ya utiifu isipokuwa ni kwa msaada wa Mwenyezi Mungu) [ Imepokewa na Abu Daud.], (Ewe Mola! Mimi najilinda kwako ni sipotee au nipoteze, au niteleze au niwafanye watu wateleze, au nidhulumu au nidhulumiwe, au nikosee au nikosewe) [ Imepokewa na Abu Daud.].

- Na amtaje Mwenyezi Mungu anapokwenda msikitini kwa kusema: (Ewe Mola! Nijaalie nuru moyoni mwangu, na nuru kwenye ulimi wangu, na nuru kwenye masikizi yangu, na nuru kwenye maangalizi yangu, na ujaalie nuru nyuma yangu, na nuru mbele yangu, na ujaalie nuru juu yangu na nuru chini yangu. Ewe Mola! Nipe nuru) [ Imepokewa na Muslim.].

5. Kwenda msikitini kwa utulivu na upole

Kwa kauli yake Mtume ﷺ: (mkisikia swala inakimiwa, nendeni kuswali, na kuweni na utulivu [ Sakinah: Utulivu na upole katika kwenda.] na umakini [ Waqaar: Umakini, utulivu, uinamishaji macho na uchache wa kuzungukazunguka.], na msiende haraka, mnachokipata kiswalini na kinachowapita kitimizeni) [Imepokewa na Bukhari na Muslim.].

6. Kumtaja Mwenyezi Mungu wakati wa kuingia na kutoka msikitini

- Atangulize mguu wake wakulia wakati wakuingia msikitini na aseme: (Najilinda kwa Mwenyezi Mungu Mkubwa, na kwa uso wake mtukufu na mamlaka yake ya tangu na tangu, kutokana na Shetani aliyefukuzwa kwenye rehema ya Mwenyezo Mungu) [Imepokewa na Abu Daud.], (Na ingia kwa jina la Mwenyezi Mungu na kumuombea rehema na amani Mtume wa Mwenyezi mungu) [Imepokewa na Muslim.]. ( Ewe Mola! Nifungulie milango ya rehema zako) [Imepokewa na Muslim.].

- Na atangulize mguu wake wakushoto wakati wa kutoka msikitini na aseme: ( Natoka kwa jina la Mwenyezi Mungu na kumuombea rehema na amani Mtume wa Mwenyezi Mungu. Ewe Mola! Mimi nakuomba fadhila zako. Ewe Mola! Nilinde mimi kutokana na Shetani ) [Imepokewa na Bukhari na Muslim.].

7. Asikae mpaka aswali rakaa mbili

Kwa kauli yake Mtume ﷺ: ( Anapoingia mmoja wenu msikitini, aswali rakaa mbili kabla hajakaa) [ Imepokewa na Abu Daud.].

8. Kujiepusha na kushikanisha vidole

Kwa kauli yake Mtume ﷺ: (Anapotawadha mmoja wenu vizuri kisha akatoka kukusudia msikitini, basi na asivishikanishe vidole vyake kwakuwa yeye yuko katika Swala) [Imepokewa na Abu Daud.]

9. Kujishughulisha na kumtaja Mwenyezi Mungu

Kujishughulisha kumtaja Mwenyezi Mungu, kuomba dua na kusoma Qur›ani wakati wa kungojea Swala bila kuwafanyia fujo wenye kuswali.

10.Kuwa mnyenyekevu katika Swala

Unyenyekevu ndio kiini cha Swala na roho yake. Swala bila ya unyenyekevu wala kuhudhurisha moyo ni kama mwili uliokufa. Ibnu Rajab, Mwenyezi Mungu amrehemu, alisema: “ Asili ya unyenyekevu ni moyo kulainika na kuwa nyororo, kutulia, kuwa mnyonge, kujivunjavunja na kupishika. Basi moyo ukinyenyekea viungo vyote huufuata moyo, kwa kuwa hivyo vinauandama na kuufuata moyo” [ Al-Khushuu’ cha ibnu Rajab.].

Basi unyenyekevu mahali pake ni moyo, na ulimi wake wenye kueleza ni viungo.

11. Kujilazimisha na Sunna ya Mtume ﷺ katika swala yake yote

Swala ni ibada ambayo ni lazima kufuata, kusifanywe chochote wala kusisemwe lolote katika Swala ambalo Mtume ﷺ hakulifanya wala hakulisema, kwa neno lake Mtume ﷺ: (Swalini kama vile mlivyoniona nikiswali) [Imepokewa na Bukhari. ]



Vitambulisho: