JIBU: Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho. Shukran kwa swali lako kuhusu kudaiwa deni la hospitali na kutaka kujua kiwango chako cha kutoa Zakaah. Mwanzo inafaa tuelewe kuwa Zakaah kama ‘Ibaadah ina masharti yake ya kutimizwa kabla ya mtu kupaswa kutoa Zakaah. Na mojawapo ya sharti ni kuwa na Nisaab (kiwango cha chini cha akiba uliyonayo), ambacho ni sawa na kununua gramu 82 za dhahabu. Kulingana na hesabu zako ni kuwa kwa sasa wewe wadaiwa takriban $ 11,500. Hivyo huna akiba ya aina yoyote ile kwa ajili hiyo wewe kishari’ah hupaswi kutoa Zakaah bali unatakiwa upewe Zakaah za kukusaidia kulipa deni hilo lako. Allaah Aliyetukuka Anasema: “Wa kupewa sadaka ni mafakiri, na masikini, na wanaozitumikia, na wa kutiwa nguvu nyoyo zao, na katika kukomboa watumwa, na wenye madeni, na katika Njia ya Allaah, na wasafiri. Huu ni waajibu uliofaridhiwa na Allaah” (at-Tawbah [9]: 60). Tunamuomba Allaah Aliyetukuka Akufanyie sahali kulilipa deni hilo kwa haraka iwezekanavyo. Na Allaah Anajua zaidi