Mbwa Wa Kufuga Je, Ni Najsi?

SWALI: Asalam alaykum kwa uwezo wa allah nimejaaliwa kuwepo nchini china kwa ajili ya masomo hata hivyo nimekutana na waislam wa nchi nyingine mbalimbali ambapo siku moja muislamu mwenzangu kutoka India nilimkuta kapakata mbwa nami nilimshangaa hata hivyo nilipomuuliza juu ya kunajisika kwa kufanya hivyo alinijibu mbwa wa mazoea (wa kufuga) hana najisi sikumpinga ila sikuridhika na jibu hilo hivyo naomba ufafanuzi naomba ikiwezekana nipate jibu kwa kupitia email yangu

JIBU: Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho. Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu unajisi wa mbwa wa kufuga. Mbwa mwenyewe hawezi kusemwa ni najisi kwa kutokuwa na dalili ya hilo, isipokuwa mate yake na majimaji ya puani mwake yanachukuliwa ni najisi kishari’ah ikiwa ni wa kufuga au vinginevyo kwa dalili iliyopatikana kutoka katika Hadiyth. Na kwa hivyo chombo chochote ambacho kitarambwa na mbwa kinapaswa kutwaharishwa kwa kuoshwa mara saba bila kutofautisha ni mbwa gani aliyekiramba, mojawapo kwa mchanga. Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ‘anhu) amesema, Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Kukitwahirisha chombo kilichorambwa na mbwa kunafanywa kwa kuosha mara saba, mojawapo kwa udongo” (Ahmad, Muslim, Abu Daawuud na al-Bayhaqiy). Na ikiwa ataramba chombo chenye chakula kikavu, kile chakula kilichoguswa na mdomo wa mbwa na kilicho pembezoni mwake kinatakiwa kitupwe, ama kilichobaki ni twahara kinaweza kubakishwa. Ama manyoya ya mbwa yakiwa makavu ni twahara. Sehemu iliyo najisi ya mbwa ni ule mdomo wake kwa ajili ya umandemande. Hivyo, mtu kucheza na mbwa au kumpakata na kumfanya ni kichezeo, si jambo lenye kushauriwa kwa kupatikana uwezekano wa kunuswa au kurambwa nguo yake na maeneo ya kuswalia na sehemu mbalimbali za nyumba yake. Mbwa si kama paka, hivyo si jambo zuri watu kuiga tabia za wasio Waislamu na wao kuanza kufuga mbwa wa vichezeo na kuwafanya kama paka. Muislamu hata akibidi kuwa na mbwa wa ulinzi, anapaswa amweke nje ya nyumba; uani au sehemu ambayo si ndani ya nyumba ili kuepuka kutiliwa najisi vyombo, nguo na sehemu za kufanyia 'ibaadah. Bonyeza viungo vifuatavyo upate maelezo zaidi: Jinsi Ya Kuondosha Najisi Ya Mbwa Kwenye Nguo Kwa Nini Nguruwe Na Mbwa Haraam? Na Allaah Anajua zaidi




Vitambulisho: