Kutengeneza Au Kupunguza Ndevu Kunaharibu Swawm?

SWALI: Asalam Aleykum Warahmat Taalah wa barakatuhu, Kwanza ni kuwatakia kheri na baraka za mwezi huu mtukufu wa ramadhani, na ALLAH atukubalie saumu zenu, Inshaa ALLAH, Swali ni kuwa, ikiwa mtu atazisawazisha ndevu kwa mkasi, siyo kunyoa au kupunguza sana na yeye amefunga mwezi hu wa ramadhani, jee saumu yake imeharibika??

JIBU: Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho. Tunamshukuru ndugu yetu ambaye ameuliza swali hili ambalo linampatia mtu sifa ya uume wake. Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amehimiza sana kuhusu kuacha ndevu na kupunguza masharubu katika Hadiyth ambazo zimenukuliwa na Maimaam kama Al-Bukhaariy, Muslim, Abu Daawuwd, At-Tirmidhiy, Maalik na wengineo. Kuweka ndevu ni Sunnah iliyo Waajib na ni jambo lenye kumpatia mtu heshima katika jamii na ni alama ya uanaume. Ndevu kama nywele ni lazima zikirimiwe na kuwekwa katika hali nzuri kwa kuchanwa na kupakwa mafuta. Haifai kuwa na ndevu kisha zikawa haziangaliwi inavyotakiwa. Katika mas-alah ya kupunguza ndevu yapo maelezo ya Ibn ‘Umar (Radhiya Allaahu 'anhuma) ambayo inasema kuwa alipokuwa akimaliza ‘Umrah au Hijjah basi huzishika ndevu zake kwa mkono wake na chochote urefu wa kiganja chake kilichozidi hukipunguza kwa kukata sehemu hiyo ya ndevu iliyozidi saizi ya mkono (Al-Bukhaariy na Maalik). Hata hivyo, Wanachuoni wanaeleza kuwa hakuna Hadiyth kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) mwenyewe inayoashiria au kuruhusu kupunguza ndevu, bali zinaashiria kuzifuga, kuziachia, kuzikuza n.k. Kusawazisha ndevu au kupunguza hakumfungulishi mtu Swawm yake. Na Allah Anajua zaidi




Vitambulisho: