Kupiga Mswaki Kwa Kutumia Dawa (Toothpaste) Kunabatilisha Swawm?

SWALI: Assalaam Alaykum warahmatu LAAHI Wabarakatu. Swali langu ni kama linavojieleza hapo juu kwenye kichwa cha hahari kuhusu kupiga mswaki kwa kutumia dawa ya colgate au dawa yeyote ile,kusema kweli hili suala limeulizwa na watu wengi sana na nyinyi mashehe zetu munalipeleka kwenye category ya kitu kinachobatilisha swaum, kwa maana hiyo hili suala halipo kabisa kwenye category hiyo, sasa tunakuombeni mtujibu hili tu ili tujue inafaa au laa. Wabillahi Taufik, Massalaam.

JIBU: Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho. Tunashukuru kwa Swali lako kuhusu kutumia dawa ya meno katika Swawm. Hakuna makatazo ya kutumia dawa ya meno wakati unapiga mswaki ukiwa kwenye Swawm, ingawa kujiepusha kuitumia wakati wa Swawm ni bora ili usije kuimeza wakati unaitumia. Na vizuri zaidi kutumia miswaak aliyokuwa akitumia Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa alihi wa sallam). Lakini ikiwa haikupatikana, na kuna haja ya kutumia dawa, basi hakuna neno kusafisha meno kwa dawa ya meno. Na kufanya hivyo hakubatilishi Swawm. Lakini inapasa kuchukua tahadhari dawa isifike kooni na kuimeza ikabatilisha Swawm. Na Allaah Anajua zaidi




Vitambulisho: