JIBU: Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho. Kukhasimiana ndugu wa Kiislamu ni jambo la hatari sana ambalo halipasi kabisa, ikiwa ni katika mwezi wa Ramadhaan au siku za kawaida. Hatari yake ni kwamba 'amali za mja anazozitenda huwa hazipokelewa na Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) hadi wapatane. Hii ni kutokana na usimulizi ufuatao ambao ni Hadiyth Swahiyh: : عن أبي هريرة رضي الله عنه قال : قال رسول الله صلى الله عليه وسلم : (( تُعرض الأعمال في كل أثنين وخميس فيغفر الله لكل أمريء لايشرك بالله شيئاً، إلا إمرءاً بينه وبين أخيه شحناء فيقول : اتركوا هذين حتى يصطلحا(( رواه مسلم Imetoka kwa Abu Hurayrah رضي الله عنه kwamba kasema Mtume صلى الله عليه وآله وسلم (('Amali njema (vitendo vyema) huoneshwa kila Jumatatu na Alkhamiys, kisha Allaah Humghufuria kila mtu asiyemshirikisha kitu Allaah, isipokuwa mtu aliyekuwa baina yake na baina ya ndugu yake uhasama, Husema: Waacheni hawa wawili mpaka wapatane)) [Muslim] Tunaona kwamba 'amali huorodheshwa na Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Hazitazami 'amali za waliogombana na juu ya hivyo Hawaghufurii madhambi yao hao wawili. Sasa ikiwa mwezi huu unajulikana kuwa ni mwezi wa Maghfirah na tunategemea kutoka tukiwa tumeghufuriwa madhambi yetu, itakuwaje ndugu hao wawili wasikhofu kukosa kusamehewa madhambi yao? Je hawaoni kwamba huenda kukaa kwao na njaa na kiu huenda kukawa ni bure ikiwa hawatafuata maamrisho haya? Hatari zaidi ni kwamba mwenye kukhasimiana na mwenziwe zaidi ya siku tatu bila ya kupatana naye, pindi yakimfika mauti akiwa katika hali hiyo basi atakosa kuingia Peponi, bali atakuwa ni mtu wa kuingizwa motoni: عن أبي أيوب الأنصاري رضي الله عنه قال : قال النبي صلى الله عليه وسلم : (( لا يَحِلُّ لِمُسْلِمٍ أَنْ يَهْجُرَ أَخَاهُ فَوْقَ ثَلَاثِ لَيَالٍ ، يَلْتَقِيَانِ فَيُعْرِضُ هَذَا وَيُعْرِضُ هَذَا ، وَخَيْرُهُمَا الَّذِي يَبْدَأُ بِالسَّلامِ .(( رواه البخاري ومسلم و في رواية أبو داود بإسناد على شرط البخاري ومسلم ((فَمَنْ هَجَرَ فَوْقَ ثَلاَثٍ فَمَاتَ دَخَلَ النَارَ )) Imetoka kwa Abu Ayyuub Al-Answariy رضي الله عنه ambaye alisema: Kasema Mtume صلى الله عليه وآله وسلم: ((Haimpasi Muislamu amhame ndugu yake zaidi ya siku tatu hata wanapokutana huyu anamgeuzia (uso) huyu na huyu anamgeuzia (uso) huyu. Na aliye mbora wao ni yule anayeanza kutoa salaam)) [Al-Bukhaariy na Muslim. Na katika Riwayaah ya Abu Daawuud ((Atakayemhama (mwenzake) zaidi ya siku tatu akafariki basi ataingia motoni))