Kumfanyia ‘Umrah Baba Yake - Je Kuna Muda Fulani Wa Kungojea Baada Ya Kutekeleza Yeye Kwanza #039;Umrah Yake?

SWALI: A/A warahmatullah wabarakatu suala langu ni hili je naruhusiwa kumfanyia mzee wangu umra baada ya mimi kumaliza umra yangu na iwapo nina ruhusiwa kuna muda fulani wakungoja? Au naweza kufanya tu nikimaliza na jee kuna masharti yoyote nafaa niyajue naomba jawabu sisi tunawategemea nyinyi ndugu zetu kutuongoza na iwapo sijibiwi email yangu ndio nimo kwenye kiza ahsantum SWALI LA PILI: Asalaam allaykum wa rahmatullah Mimi nina nia ya kwenda umra je nikimaliza umra yangu naweza kumfanyia mzee wangu aliyefariki umra? Na ikiwa yawezekana naweza kumfanyia nikimaliza tu umra? Au mpaka nisubiri siku kadhaa? Au kuna masharti yoyote yafaa niyajue. Suali la pili kuhusu ihram je naweza kuvaa nguo yoyote ya stara au mpaka nivae ihram? Shukran

JIBU: Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho. Shukrani kwa swali lako kuhusu kumfanyia ‘Umrah baba yako. Kwanza ushauri kwako na kwa wengine wenye tabia ya kufupisha salaam, ni bora liepukwe hilo kwani ni kujikoseshea fadhila nyingi zinazopatikana katika kusalimiana, kadhaalika unaweza usieleweke kwa vifupisho hivyo na isitoshe havileti maana. Ni jambo la busara kwa mtoto kumkumbuka na kumfanyia ‘Ibaadah mzazi wake ambazo hakuweza kuzifanya kwa sababu moja au nyingine ili mizani yake ijae. Moja ya ‘amali ambayo mtoto anaweza kumfanyia baba yake ni ‘Umrah au Hajj. Na ‘amali hizi huwezi kuzichanganya na pia huwezi kuzifanya kabla ya wewe kutekeleza ‘amali hiyo. Baada ya kumaliza ‘Umrah yako inabidi upunguze nywele na utoke katika ihraam, kisha utakwenda Tan’iym katika Masjid ‘Aaishah ambapo utatia Niyay na kuvaa tena ihraam ile uwe ni mwenye kumfanyia baba yako ‘Umrah. Hata hivyo, ukiwa na uwezo itakuwa bora zaidi baada ya wewe kutekeleza Hajj, mwaka unaofuata au utakapojaaliwa mbeleni ujitahidi umfanyie baba yako Hajj ikiwa hakufanya. Hajj si kama ‘Umrah ambayo unaweza kuifanya zote mbili kwa mwaka mmoja. Zaidi unaweza kutembelea Fataawa mbalimbali kuhusiana na Hajj pamoja na makala na mafundisho mbalimbali ha chini: Fataawa Za Hajj Na Umrah Hajj Na Allaah Anajua zaidi




Vitambulisho: