JIBU:
Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.
Shukran kwa swali lako kuhusu kukimu katika Swalaah tofauti – za faradhi na Sunnah.
Hakika ni kuwa Iqaamah ni kwa ajili ya Swaalah ya faradhi peke yake na si Sunnah, kwani kinachotakikana ni kuwa Swaalah hiyo ya faradhi ijulishwe kuwa itayari na watu nao waanze kujipanga kwenye Swafu.
Ama Swaalah za Sunnah kila mtu huswali peke yake, na ni uzuri mtu kuziswalia nyumbani kwake hivyo hakuna haja ya Iqaamah kwani hakuna mwenye haja ya kujulishwa kujitayarisha au kupanga Swafu kwani kila mtu anajiswalia peke yake.
Inatakiwa baada ya Kuadhiniwa ndio unaswali Qabliyah, kisha baada ya hapo ukifika wakati wa Kuqimiwa kunaqimiwa na kuswali Swalaah ya faradhi. Na baada ya Swalaah ya fardh unafanya dhikr kisha unaswali Swalaah ya ba’adiyah kama ni Adhuhuri au Magharibi au ‘Ishaa.
Na hata ikiwa Swalaah ya Sunnah inaswaliwa kwa Jama’ah kama vile Swalaah ya Taraawiyh, hakuna Iqaamah kwani Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hakufanya hivyo au kutufundisha sisi tufanye hivyo.