Kufungua Swawm Mapema Katika Miji Ya Afrika Mashariki

SWALI: Assalamu Aleikum warahmatullahi wabarakatuhu, Bismillahi Rahmanir Rahim, Sifa njema zote zote ni stahiki ya Mwenyezi Mungu (S.W.), rehma za Mwenyezi Mungu na Amani Yake iwe juu ya Mjumbe wake Mtukufu Muhammad (S.A.W.W). Ama baada ya hayo yaliyotangulia mimi ninataka kuuliza kuwa kwanini tunatumia hadithi ambazo zinaamrisha watu wawahi kufungua katika mwezi mtukufu wa Ramadhani, wakati katika Qur'an Mwentezi Mungu Anasema "Na kamilisheni Funga mpaka usiku". Sasa kwa nini siku hadithi zinazosema kuwa watu wafungue mapema kiasi ambacho katika miji yetu hii ya Afrika ya Mashariki watu wanafungua wakati mwenine kuanzia saa 12:18! Sasa hii sio hatari! kwa nini tusifungue wakati ambapo giza ndio linaanza kuingia? Na jee hii hadithi inayoamrisha watu "waharakishe kufungua" ni sahihi kweli? Si maneno yaliyotungwa na maadui wa uislamu ili kupotosha na kuharibu ibada za waislamu? Hilo ndilo swali langu.

JIBU Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho. Shukrani kwa swali lako kuhusu kufungua mapema kama ulivyoelezea kwa uoni wako mwema. Kwanza tunapenda kukukumbusha unapomtaja Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) na kumtukuza, na kumtaja Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na kumuombea rahma na amani, basi andika kwa utajo uliokamilika na unaofahamika badala ya kuandika kwa ufupi (S.W.), au (S.A.W.W)., kumbuka hiyo ni heshima zaidi na mapenzi zaidi. Tunaweza kuandika mambo mengine kwa urefu yakaeleweka lakini tunapomtukuza Allaah na tunapomuombea kipenzi chetu tunamfupishia. Hivyo, haifai na haipendezi. Hakika ni kuwa suala limewachanganya wengi na hasa Mashia mpaka wakalielewa vingine kwa njia isiyokuwa ya sawa. Neno ambalo limewaletea utata watu ni lile ambalo liko katika Qur-aan: “Thumma atimmusw Swiyaama ilal Layl”. Al-Layl maana yake ni usiku. Nani anaweza kuelezea maana ya usiku inavyopaswa kufahamika katika Aayah hiyo? Aliye na nafasi nzuri ya kuelezea maana ya usiku ni Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) si mwengine yeyote. Yeye ndiye aliyeweza kutubainishia hadd (adhabu) ya mwizi mwanamme na mwanamke pale Allaah Aliposema: “Na mwizi mwanamume na mwizi mwanamke, ikateni mikono yao” (al-Maa’idah [5]: 38). Naye (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akatuelezea wa kukatwa si mkono mzima bali kiganja hadi sehemu ya kiwiko Aayah hiyo iliyopo juu inaamrisha kufturu/kuftari jua linapokuchwa. Imenukuliwa katika Swahiyh mbili kuwa Mtume wa Allaah (Swalla llaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisema: “Usiku unapokuja kutoka upande huu (Mashariki) na mchana unapoondoka kutoka upande huu (Magharibi, hivyo mfungaji hufturu”. Na kuhusiana na usiku Hadiyth iliyopokewa na al-Bukhaariy na Muslim kutoka kwa Ibn Abi Awfaa (Radhiya Allaahu ‘anhu) ambaye amesema: “Tulikuwa pamoja na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) katika safari. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimwambia mtu mmoja: ‘Teremka ututengenezee sawiq (aina ya chakula kinachotengenezwa na unga ngano au shayiri na sukari au tende) na maji kwa ajili yangu’. Mtu huyo akasema: ‘Jua halijakuchwa, Ewe Mtume wa Allaah!’ Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamwambia tena: ‘Teremka ututengenezee sawiq na maji kwa ajili yangu’. Mtu huyo akasema: ‘Jua halijakuchwa, Ewe Mtume wa Allaah!’ Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema tena kwa mara ya tatu: ‘Teremka ututengenezee sawiq na maji kwa ajili yangu’. Mtu huyo aliteremka na kumtengenezea sawiq na maji kwa ajili yake. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikunywa kisha akaashiria kwa mkono wake upande wa Mashariki na kusema: ‘Ukiuona usiku unaingia upande huo, hivyo mfungaji ashafungua”. Na kuna fadhila ya kufuata agizo lingine la Mtume (Swalla llaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) pale alipowaamrisha Waislamu wafungue mapema kama anavyoelezea Sahl bin Sa’d (Radhiya Allaahu ‘anhu): “Watu watabaki kwenye kheri madhali wanafanya haraka kufturu” (al-Bukhaariy na Muslim). Na Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ‘anhu) amemnukuu Mtume (Swalla llaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akisema: “Allaah Aliyetukuka Anasema, ‘Wapenzi kwangu miongoni mwa waja Wangu ni wale wanaofanya haraka kufturu” (Ahmad). Kwa hivyo, Hadiyth zote hizi zilizo Swahiyh zinaelezea neno al-Layl ambalo ikiwa tutalifahamu kwa maana hiyo hakutakuwa na utata wa aina yoyote ile. Wengi hutiwa mashaka na Mashia ambao wameelewa suala hilo kinyume kama walivyoelewa masuala mengi kinyumenyume au kwa tafsiri zao wanazotaka wenyewe kwa kutekeleza na kutimizia matashi yao. Na Allaah Anajua zaidi




Vitambulisho: