Kufuliwa Nguo Na Wakristo

SWALI: Assalam alaykum warahmatullah wabarakatuh, Allah awazidishie na awafungulie milango ya kheri,nimefaidika sana na hii web yenu. Swali: Waislamu wengi wana mahausigeli wa kikiristo na hata kama sio wakiristo lkn wengi wao sheria za dini hawazijui, je itakuwaje kwa kuwa hawajui twahara na huwafulia nguo zao ambazo huzitumia ktk swala? Je inajuzu? Wabillah Tawfiq

JIBU: Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho. Kama tunavyosema mara nyingi ya kwamba Uislamu umetupatia majibu ya maswali yetu, kwani ni mwongozo kamili kwa mwanadamu. Kuhusu suala hili hapana tatizo lolote kwani Allah Ametuambia hata vyakula ambavyo wanavipika ni halali kwetu kwa hivyo tusijitie dhiki kwani Muumba wetu Anawajua zaidi kuliko tunavyowajua sisi: “Leo mmehalalishiwa kila vilivyo vizuri. Na chakula cha walio pewa Kitabu ni halali kwenu, na chakula chenu ni halali kwao” (5: 5). Sasa ikiwa chakula chao ni halali, seuze kufuliwa nguo. Ukitazama katika maisha ya Mtume (s.a.w.w) na Maswahaba zake (r.a.) utakuta ya kwamba walikuwa na wajakazi na vijakazi wasiokuwa Waislamu na haikuwa shida yoyote kwao. Na Allah Ametufanyia mambo sahali katika kupelekesha maisha yetu hapa duniani bila ya kwenda kinyume na maadili yetu ya Kiislamu. Na hasa wakati huu wetu ambapo vipo vifaa vya kufanyia usafi vingi ambavyo wanaweza kutumia katika kuhakikisha unadhafa. Na hasa ukizungumzia kuhusu kufua nguo basi nguo zinatiwa katika maji na sabuni na kutolewa povu kwa kutiwa katika maji. Njia hiyo nguo zinakuwa hazina tatizo lolote. Na wewe kama Muislamu unaweza kumfundisha yale unayoyataka na hata ni fursa ya kumueleza kuhusu Uislamu na huenda akaukubali ukweli na kuingia katika Dini hii tukufu. Na nasaha kwa kila mmoja ni kuwa katika nchi zetu wapo kina mama au wasichana ambao ni hohe hahe, hawana mbele wala nyuma, nao wako katika harakati ya kutafuta kibarua. Hivyo, katika kupatiana kazi mwanzo tuangalie kama utapata hausigeli (house girl) wa Kiislamu na ikiwa utapata basi itakuwa kheri zaidi kwani utakuwa unampatia mshahara ambao ataweza kujisaidia nao yeye na familia yake. Na pia tutazame mishahara tunayowapa hao wafanyakazi wa nyumbani iwe inalingana kwa karibu na mahitaji ya hali ya maisha na tusiwapunje wala kuwatumia kwani hakika wao ni kama familia; wanakupikia, wanakufulia, wanakupigia deki au huva (hoover) wanakutandikia vitanda vyenu, wanawalelea watoto wenu n.k. Kwa hiyo wanastahiki kulipwa vizuri na kuwatazama. Bila kusahau kula nao pamoja na si kuwatenga wao wakawa wanakula peke yao jikoni. Na hali hiyo itampatia faraja kubwa na kujihisi kama ni kiungo cha familia, na pia kama si Muislam, basi atavutika na Uislam, kwa sababu Uislam ni matendo na akhlaaq. Na Allah Anajua zaidi.




Vitambulisho: