Ni kitu anachokiweka mwenye kuswali mbele yake, baina yake yeye na mwenye kupita mbele yake
Ni kitu anachokiweka mwenye kuswali mbele yake, baina yake yeye na mwenye kupita mbele yake
Kuweka kizuizi kumeamrishwa na Sheria, mjini na safarini, kwa Swala ya faradhi na swala ya Sunna, msikitini na mahali penginepo, kwa hadithi iliyothubutu kwa Mtume ﷺ kwamba yeye alisema: ( Anaposwali mmoja wenu aelekee kwenye kizuizi na awe karibu nacho) [ Imepokewa na Abu Daud.].
Amepokewa Wahb (R.A.) kuwa alisema: (Mtume alituongoza katika Swalah hapo Mina, akaisimamisha fimbo yake ﷺ – nayo ni kipande cha mti kidogo- mbele yake, akatuswalisha rakaa mbili) [ Imepokewa na Ahmad.].
Kuweka kizuizi ni lazima, kwa kuwa Mtume ﷺ ameamrisha kuweka kizuizi kwa imamu na pia mwenye kuswali peke yake na amehimiza hilo. Kwa hivyo inatakikana kwa Muislamu aweke kizuizi mbele yake aswalipo na amzuie mwenye kupita baina yake yeye na kile kizuizi alichokiweka, kwa kauli yake Mtume ﷺ: (Usiswali isipokuwa uwe umeelekea chenye kukuzibia, na usimuache yoyote kupita mbele yako, na akikataa basi pigana naye) [ Imepokewa na Ibnu Khuzaimah.].
Mwenye kuswali ametakiwa na Sheria aweke kizuizi kwa hekima nyingi miongoni mwazo:
1. Kumzuia mtu asipite mbele ya mwenye kuswali akamkatia unyenyekevu wake.
2. Kummakinisha mwenye kuswali aishughulishe akili yake kwenye lile jambo la Swala na sio jambo lingine.
3. Ajihifadhi na kukatikiwa na swala yake kwa kupita mwanamke au mbwa au punda mbele yake, kwa hadithi iliyopokewa na Abu Dharr t kuwa alisema kwamba mtume ﷺ alisema: (Mmoja wenu akiinuka kuswali, kinatosha kuwa ni kizuizi chake iwapo mbele yake pana mfano wa kiwekea miguu kwa mwenye kupanda mnyama. Iwapo hakuna mbele yake mfano wa kiwekea miguu, basi Swala yake huharibiwa na punda, mwanamke na mbwa mweusi”. Nikasema: Ewe Abu Dharr! Kuna tofauti gani ya Mbwa mweusi na mbwa mwekundu na mbwa manjano? Akasema: Ewe mtoto wa ndugu yangu! Nilimuuliza Mtume wa Mwenyezi Mungu ﷺ kama ulivyoniuliza, akasema: “Mbwa mweusi ni Shetani”) [ Imepokewa na Muslim.].
1. Kuweka kizuizi ni kwa imamu na mwenye kuswali peke yake. Ama maamuma, kizuizi cha imamu ni kizuizi chake. Amepokewa Ibnu Abbas t akisema: (Nilikuja nimepanda punda [ Ataan: punda jike.], na mimi siku hiyo nimekaribia umri wa kubaleghe na Mtume wa Mwenyezi Mungu ﷺ yuwaswalisha watu hapo Mina, nikapita mbele ya sehemu ya safu, nikashuka na nikamuacha punda kulisha, nikaingia safuni na hakuna mtu yoyote aliyepinga) [Imepokewa na Bukhari na Muslim.].
2. Haifai kupita mbele ya mwenye kuswali, kwani hilo ni miongoni mwa dhambi kubwa, kwa neno lake Mtume ﷺ: (Lau anajua dhambi alizonazo mpitaji mbele ya mwenye kuswali, ingalikuwa ni bora kwake kungojea siku arubaini kuliko kupita mbele yake). Abunnadhr anasema: ” Sijui kama alisema “siku arubaini” au “miezi” au “miaka” [ Imepokewa na Bukhari na Muslim.].
Isipokuwa iwapo kule kupita ni kando ya pale mahali pa kusujudu kwake ikiwa mwenye kuswali ameweka kizuizi.
3. Ni lazima kwa mwenye kuswali amzuie anayepita mbele yake. Abu Said al- Khudri t alipokewa akisema: Nilimsikia Nabii ﷺ akisema: (Anaposwali mmoja wenu kuelekea kitu alichokifanya ni kizuizi chake cha kumzuia na watu, akaja mtu kutaka kupita mbele yake basi amzuie kupita, na akikataa, basi apigane naye, kwani yeye ni Shetani) [ Imepokewa na Bukhari na Muslim.].
4. Kuna jopo la wanavyuoni waliyouvua Msikiti wa Haram, wakawaruhusu watu kupita mbele ya mwenye kuswali, kwa dalili ya kutomtia mtu makosani, kwa kuwa kuwazuia watu. kupita mbele ya mwenye kuswali kwenye Msikiti wa Haram ni kumtia mtu madhambini na mashakani mara nyingi.
5. Na kizuizi cha Swala hupatikana kwa kuswali kuelekea ukutani au kwenye nguzo miongoni mwa nguzo za msikiti au kabati au aweke kitu mbele yake kama vile fimbo na mfano wake.
6. Masafa baina ya mwenye kuswali na kizuizi yanakadiriwa kwa nafasi ya kupita mbuzi, kwa hadithi iliyopokewa na Sahl akisema: ( Baina ya mahali mtume wa Mwenyezi Mungu alipokuwa akiswali na baina ya ukuta ni kiasi cha kupita mbuzi) [Imepokewa na Bukhari na Muslim.].
Hakuna, katika hadithi iliyopita kuwa kupita mwanamke humuharibia mtu Swala, kumfananisha mwanamke na punda na mbwa mweusi. Vitu vitatu kutajwa kwenye mfumo mmoja haina maana kuwa sababu zake za kuharibu Swala zinafanana. Yaani haimaanishi kuwa sababu ya kuwa mbwa mweusi anamuharibia mtu Swala kuwa ni sababu hiyohiyo inayofanya punda na mwanamke wamuharibie mtu Swala.
Hivyo basi, kule kuwa mbwa mweusi ni Shetani, kama hadithi ilivyosimulia, haina maana kuwa punda au mwanamke ni Shetani. Huenda zikawa sababu ya hivi vitatu ni tafauti ingawa vimekusanywa kwenye mfumo mmoja, ingawa sababu ya mbwa imeelezwa wazi kwenye tamko la hadithi, na sio vingine vilivyosalia. Hii inaonyesha kuwa sababu yake ni tofauti na sababu za vile visalievyo na haifanani nazo.
Na inamkinika kutoa sababu ya kuwa mwanamke anamkatia mwenye kuswali Swala yake kwa kupita mbele yake, au karibu yake , ni kuwa hilo huenda likambabaisha mwanamume moyo wake na huenda likamshughulisha na Swala. Kwa ujumla, kupita kwa mwanamke kunaushughulisha zaidi moyo wa mwanamume kuliko kupita mwanamume mwingine. Hivyo basi, na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi zaidi, amri ya Sheria imekuja kuwa yeye ni miongoini mwa vitu vinavyoharibu Swalah ya mtu, ili kuhifadhi unyenyekevu wa Swala.