Kipi Kiwango Cha Zakaah, Je, Inafaa Kutolewa Kwa Ajili Ya Madrasa?

SWALI: Assalaam alaikum Sheikh. Mimi nataka kujua mwanzo wa kiwango cha kutoa zakaah, kwa ile mali iliyopitikiwa na mwaka? Jee inafaa zakaah kupeleka kwa Madrasa ya Kiislam badala ya kuwapa maskini na fukara? Mwisho masheikh tunashukuru sana kwa majibu yenu na INSHAALLAH akuzidishieni zaidi kwa hay

JIBU: Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho. Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu kiwango cha Zakaah na ikiwa inafaa kutolewa Zakaah kwa Madrasah. Ama kiwango ambacho mtu akiwa nacho inabidi atoe Zakaah ni kuwa na pesa zilizo sawa na thamani ya gramu 82.5 za dhahabu kwa kiwango cha chini kabisa. Kwa njia rahisi unaweza kuulizia katika nchi unayoishi kuhusu thamani ya dhahabu kwa sasa. Ukisha kupata thamani hiyo utajua jumla ya gramu hizo bila ya shida yoyote. Ama swali lako la pili haliko wazi sana lakini tunatumai kwa majibu haya ambayo tutayatoa yatalenga katika lile unalokusudia. Ikiwa ni kujenga Madrasah yenyewe itakuwa haifai kufanya hivyo kwa pesa za Zakaah. Kwa ajili hiyo itabidi matajiri miongoni mwa Waislamu na hata Waislamu wa kawaida kila mmoja kwa uwezo wake achangie katika ujenzi huo. Na kufanya hivyo itawafanya wenye kuchangia kupata sadaka ya kuendelea na hivyo kupata thawabu hata wanapokufa na kuzikwa. Ama ikiwa ni kuwalipa waalimu wa Madrasah ambao hawana ajira kwani wazazi ni masikini na hawawezi kutoa ada ya Madrasah itajuzu kufanya hivyo kwani kundi moja la kupewa Zakaah ni wale ambao wako katika Njia ya Allaah, na kusomesha dini ni katika mojawapo ya njia hiyo. Ama ikiwa waalimu wenyewe hawana ujira kwa kusomesha kwao nao wenyewe ni hohehahe basi wataingia katika kundi la masikini au mafukara hivyo kuwawezesha wao kupata Zakaah hizo. Na Allaah Anajua zaidi




Vitambulisho: