JIBU: Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho. Shukrani zetu za dhati kwa swali lako. Ama kuhusu suala hili hebu tutazame Hadiyth ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) inayosema: Abu Sa'iyd al-Khudriy (Radhiya Allahu 'anhu) alimuuliza Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): "Je, twaweza kuchukua wudhuu katika kisima cha Buda'ah". Akajibu: "Maji ni twahara, hayanajisiki na chochote" (Ahmad, ash-Shaafi'iy, Abu Daawuud, an-Nasaa'iy na at-Tirmidhiy). Kwa mujibu wa Hadiyth hii maji hayo katika beseni ni twahara ila ikiwa yamebadilika moja katika sifa zake kama rangi, harufu na tamu. Ikiwa sifa yake imebadilika basi maji kama hayo hayataweza kutumika tena kwa kutawadhia. Hata hivyo, tungependa kuwanasihi ndugu na dada zetu kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amekataza watu kukojoa kwenye maji yasiyotembea ikiwa ni katika beseni, mto, ziwa, kisima, birika na kadhalika. Katazo hilo ni kuwaweka watu wawe mbali na kupatikana na magonjwa au kuudhiwa na harufu mbaya. Na Allaah Anajua zaidi