JIBU: Sifa zote njema Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allahu 'anhum jamiy'an) na watangu wema mpaka Siku ya Qiyaamah. Hakuna ubaya wowote kisheria kuchelewesha kukoga janaba: na hali kadhalika hakuna lazima ya kisheria kuharakisha kukoga janaba, japo ni bora kiunadhifu kufanya hivyo. Imepokewa riwaya kutoka kwa Abu Hurayrah (radhiya Allahu 'anhu) (Ya kwamba Abu Hurayrah (radhiya Allahu 'anhu) alikutana na Mtume (Swalla Allahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwenye mitaa ya Madiynah, huku akiwa na janaba, akarudi kinyumenyume (kwa kumkimbia Mtume (Swalla Allahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akaenda kukoga, na kuja tena mbele ya Mtume (Swalla Allahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) Mtume akamuuliza, "Ulikuwa wapi ewe Aba Hurayrah?) akasema nilikuwa na janaba, nikahisi kero kuketi nawe nikiwa si nadhifu, Mtume (Swalla Allahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema SubhaanaAllah, hakika Muislam hanajisiki" (Al-Bukhaariy Hadiyth Namba 283 na Muslim Hadiyth Namba 309). Ila ni bora zaidi kufanya wudhuu ikiwa Muislamu anataka kuchelewesha janaba kama ilivyokuja dalili katika Hadiyth zifuatazo: YA KWANZA: عن عائشةَ قالت: كان النبيُّ صلى الله عليه وسلم إِذا أرادَ أن [يأكل أو] يَنامَ وهوَ جُنُبٌ غَسلَ فَرجَهُ وتَوضَّأَ وضوءه للصلاة Imetoka kwa ‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anha) ambaye amesema: "Kila alipotaka (kula) au kulala akiwa katika hali ya janaba, (yaani baada ya kujimai na kabla ya kukoga) Mtume (Swalla Allahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akiosha sehemu zake za siri na kufanya wudhuu kama wa Swalah “[Al-Bukhaariy na Muslim] YA PILI: عن أبن عمر رضي الله عنهما أن عُمرُ قال: يا رسول الله : أَيَنامُ أحدُنا وهوَ جُنبٌ؟ قال: ((نَعمْ، إِذا تَوضَّأَ)) وفي رواية ((توَضَّأْ واغْسِلْ ذَكَرَكَ ثمَّ نَمْ)) وفي رواية ((نَعَمْ. لِيَتَوَضَّأْ ثُمَّ لْيَنَمْ، حَتَّى يَغْتَسِلَ إِذَا شَاءَ)) وفي أخرى: ((نَعَمْ، وَيَتَوَضَّأُ إِنْ شاءَ)) Imetoka kwa Ibn 'Umar (Radhiya Allahu ‘anhuma) kwamba 'Umar alisema: "Ewe Mjumbe wa Allaah, je, tulale tukiwa katika hali ya janaba?" Mtume (Swalla Allahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akajibu: ((Ndio baada ya kuchukua wudhuu)) [Al-Bukhaariy Na Muslim] Katika riwaya nyingine ((Fanya wudhuu na osha sehemu zako za siri kisha ndio ulale)) [Al-Bukhaariy Na Muslim] Na katika riwaya nyingine ((Ndio, unaweza kufanya wudhuu, kulala na kuoga unapopenda)) [Al-Bukhaariy Na Muslim] Na katika riwaya nyingine pia: ((Ndio na fanya wudhuu ukipenda)) [Ibn Khuzaymah na Ibn Hibbaan ni Swahiyh] Riwaaya ya mwisho inaonyesha kuwa wudhuu huu sio fardh. YA TATU: عنْ عَمَّارِ بنِ يَاسِرٍ ، أنَّ رَسُولَ الله صلى الله عليه وسلم قالَ: ((ثَلاَثَةٌ لاَ تَقْرَبُهُمْ المَلاَئِكَةٌ: جِيْفَةُ الْكَافِرِ، وَالمُتَضَمِّخُ بِالخُلُوقِ، وَالْجُنُبُ إلاَّ أنْ يَتَوَضَّأَ)) Imetoka kwa 'Ammaar ibn Yaasir kwamba "Mtume Swalla Allahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Watu watatu Malaika hawawakaribii; maiti ya Kafiri, mwanamume anayejitia manukato ya kike, na mwenye janaba (aliyefanya jimai) hadi afanye wudhuu)) [Abu Daawuud, Ahmad na wengine ni Swahiyh] .Na Allah Anajua zaidi
Ingia katika kiungo kifuatacho upate maelezo zaidi:
Ghuslu - Wakati Wa Mwisho Kukoga Janaba Katika Mwezi Wa Ramadhaan