Hukumu za Hija na Umra

11275

 

Hijja

Maana ya Hijja

Hija kilugha

Kukusudia na kuelekea

Hijja kisheria

Ni kukusudia Makka katika kipindi maalumu ili kutekeleza ibada ya Hijja.

Hukumu ya Hijja na fadhla zake

Hijja ni mojawapo ya nguzo za Kiislamu. Mwenyezi Mungu Alioyetukuka Ameilazimisha kwa waja wake. Anasema Mwenyezi Mungu U: {Ni haki ya Mwenyezi Mungu kwa watu waihiji Alkaba, kwa anayeweza kwenda huko. Na Mwenyezi Mungu ni Mkwasi Hawahitajii walimwengu} [3: 67]

Na amesema Mtume (saw): (Uislamu umejengwa juu ya misingi mitano: Kukubali kuwa hapana mola isipokuwa Mwenyezi Mungu na kwamba Muhammad ni mja Wake na Mtume Wake, kusimamisha Swala, kutoa Zaka, kuikusudia Alkaba kwa Hija na kufunga mwezi wa Ramadhani) [Imepokewa na Bukhari na Muslim.].

Na amsema Mtume wa Mwenyezi Mungu(saw): (Mwenye kuhiji asiseme maneno machafu [ Rafath: ni neno linalotumika kumaanisha maneno machafu.] na asitoke kwenye utiifu wa Mwenyezi Mungu [ Fusuuq: maasia.], atasamehewa dhambi zake zilizotangulia) [Imepokewa na Tirmidhi.].

Na Hijja ni lazima kwa umri mara moja.

Masharti ya Hijja

1. Uislamu

Hijja haimlazimu kafiri, na akihiji haisihi hijja yake.

2. Kuwa na akili

Hija haimlazimu mwendawazimu, kwa neno lake (saw): (Watu watatu hawaandikiwi dhambi: aliyelala mpaka azunduke, mtoto mapaka abaleghe na mwendawazimu mpaka apate akili) [Imepokewa na Abu Daud.].

3. Kubaleghe

Hijja haimlazimu mtoto mdogo, na lau mtoto mdogo atahirimia hija basi hija yake itasihi. Lakini haimtoshelezi na Hijja ya Uislamu, na itahesabiwa ni Sunna. Hii ni kwa hadithi ya Ibnu ‹Abbas t kwamba mwanamke mmoja alimuinulia Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) mtoto, na akasema: «Je, huyu ana Hija? Mtume akasema: (Ndio, nawe una thawabu) [Imepokewa na Muslim.].

Mtoto Mdogo anafaa kuhirimia Hijja

4. Uhuru

Hijja haimlazimu mtumwa, kwa kuwa Mtume (saw) amesema: (Mtumwa yoyote aliyehiji kisha akaachwa huru, basi itamlazimu Hija nyingine) [Imepokewa na Muslim.].

5. Uwezo

Nao ni kuwa na matumizi [ Zaad: Vitu anvyovihitajia kama chakula, kinywaji na mavazi.] na kipando [ Raahilah: Kipando anachokipanda kama gari au ndege au meli..], kwa neno lake Mwenyezi Mungu U: {Ni haki ya Mwenyezi Mungu juu ya watu waikusudie Alkaba kwa ibada ya Hija kwa anayeweza kwenda huko} [3: 97]

6. Kuweko na maharimu [ Mahram: ni yule ambaye ni haramu kwa mwanamke kuolewa naye kama baba, ndugu na mjomba.] ya Mwanamke

Kwa hadithi ya Ibnu ‹Abbas t kuwa alisema: Nilimsikia Mtume (saw) akisema: ( Hasafiri mwanamke isipokuwa pamoja na mtu maharimu yake).

Akainuka mtu mmoja akasema: Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! Mke wangu ametoka kwenda kuhiji, na mimi nimejisajili katika vita kadha na kadha. Akasema Mtume (saw): (Toka uende kuhiji na mkeo) [Imepokewa na Bukhari na Muslim.]

Kuhijiwa (kuwakilisha mtu)

ِ Asiyeweza kuhiji au kufanya Umra kwa uzee au maradhi yasiyotarajiwa kupoa, au kwa udhaifu katika mwili wake kwa namana ya kutoweza kupanda kipando, itamlazimu yeye amwakilishe mtu wa kumhijia au kumfanyia Umra, na hilo linamtosheleza yeye hata kama atapona baada ya kuwa ule mwakilishi wake ashahirimia kwa Hijja au Umrah. Fadhl bin ‘Abbas t Alipokewa akisema kwamba mwanamke wa ukoo wa Khath’am alisema: (Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! Baba yangu ilimjia faradhi ya Hija akiwa mzee mkongwe hawezi kulingana juu ya mgongo wa ngamia. Mtume(saw) akasema “Mhijie”) [ Imepokewa na Tirmidhi.].

Mtu asiyeweza kuhiji

Imesharutishwa kwa mtu anayemwakilisha mwingine kumuhijia masharti mawili:

1. Masharti ya Hijja yaliyotangulia yawe yamepatikana kwake.

2. Awe yule aliyewakilishwa ameshajihijia nafsi yake. Mtu lau amhijia mwingine, na yeye bado hajajihijia nafsi yake, Hija yake ya kumhijia mwingine haisihi na itazingatiwa kuwa amejihijia mwenyewe Hija ya Uislamu. Na dalili yake ni hadithi iliyothubutu kutoka kwa Ibnu ‘Abbas t kuwa Mtume (saw) alimsikia mtu akisema: (“Labeka kwa niaba ya Shubrumah”. Mtume akasema: “Ni nani Shubrumah?” Akasema: “Yeye ni jamaa yangu au ndugu yangu”. Akasema: “Je, umjihijia nafsi yako?” Akasema “La, bado”. Akasema Mtume: “Jihijie nafsi yako kisha mhijie Shubrumah”) [Imepokewa na Abuu Daud].

Umra

Maana ya Umra

Umra kilugha

Ziara

Umra kisheria

Ni kuizuru Nyumba Takatifu (Alkaba) wakati wowote mtu anapotaka, kwa kutekeleza matendo ya ibada maalumu.

Hukumu ya Umra na fadhla zake

Umra ni wajibu wa mara moja katika umri wa mtu kama vile hijja, kwa kauli yake Mtume (saw): (Uislamu ni ukubali kwamba hakuna mola isipokuwa Mwenyezi Mungu na kwamba Muhammad ni Mtume wa Mwenyezi Mungu, na usimamishe Swala, na utoe Zaka, na uikusudie Alkaba kwa ibada ya Hija na ufanye Umra, na uoge kutokana na janaba, na ukamilishe udhu, na ufunge Ramadhani) [Imepokewa na Ibnu Khuzaimah. ]

Na amesema Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw): (Umra mpaka Umra ni kafara ya dhambi baina yake, na Hija iliyokubaliwa haina malipo isipokuwa Pepo) [Imepokewa na Bukhari na Muslim.]