Fedha Inayobaki Benki Itolewe Zakaah?

SWALI: Assalamu alakykum; Natanguliza Shukrani kwa Allaah (Subhanahu wataala) kutupa neema ya uhai na kuwawezesha ndugu zetu kubuni na kuendeleza mtandao wenye manfaa kede kede. Allaah (Subhanahu wataala) ndiye mlipaji. Nina akaunti benki ambayo huwa natoa na kuweka akiba bila ya kiwango maalum. Jee kuna uwajibikaji wowote wa kuitolea Zakaah ile fedha inayobaki benki kwa kutimia mwaka. JazaaKaAllaah

JIBU: AlhamduliLlaah - Himdi Na Sifa Zote Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho. Shukrani kwa ndugu yetu kuhusu suala hili zuri katika Dini yetu Tukufu. Dini yetu inaangalia maslahi ya kila mmoja hata ya maskini. Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) Ameweka Zakaah kuwatwahirisha matajiri na kuwapatia fursa maskini waweze kusaidika na kunyanyua hali zao za kimaisha. Ifahamike kuwa fedha (pesa) zinazotolewa Zakaah na kanuni yake ni kanuni yake ni kama dhahabu na fedha. Akiba ya pesa ulizonazo benki zinatolewa Zakaah ikiwa zitafikia masharti yaliyowekwa katika hilo. Masharti ya pesa hizo kutolewa Zakaah ni: 1. Kupitiwa na mwaka wa Kiislamu. 2. Kufikia kiwango: Kiwango chake ni Dinari 20 za dhahabu. Kwa hivi sasa tunaweza kusema ni baina ya gramu 82.5 hadi 88. Kwa hiyo, ukiwa na kiwango hicho cha pesa na zikapitiwa na mwaka inabidi utoe Zakaah kwa kiwango cha 2.5%. Kutegemea na nchi uliyoko utafanya hesabu yako. Kwa mfano ikiwa gramu moja ya dhahabu ni shilingi 1000, hivyo ukiwa na akiba yako ya Shilingi 82,500. Pesa hizi zikapitiwa na mwaka mzima inafaa utoe 2.5% ya hizo pesa kuwapatia watu maalumu waliotajwa katika Qur-aan. Watu wenyewe ni kama ayah inavyosema: “Sadaka hupewa mafakiri, masikini, wanaozitumikia, wanaotiwa nguvu nyoyo zao (juu ya Uislamu), kuwapa uungwana watumwa, kuwasaidia wenye deni, kutengeneza mambo aliyoamrisha Allaah na kupewa wasafiri walioharibikiwa” (9: 60). Na Allaah Anajua zaidi




Vitambulisho: