Cheo cha Swala na Hukumu Yake

16211

 

Maana ya Swalah

Swalah kilugha

Maombi

Swala kisheria

Ni kumuabudu Mwenyezi Mungu U kwa maneno na vitendo maalumu, vinavyoanzia kwa takbiri na vinavyomalizikia kwa kupiga salamu.

Hadhi ya Swalah katika Uislamu

1. Swalah ni nguzo ya pili katika nguzo za Uislamu.

Amesema Mtume ﷺ: (Uislamu Umejengwa juu ya nguzo tano: kukiri kwa moyo na kubaini kwa ulimi kuwa hapana Mola apasae kuabudiwa kwa haki isipokuwa Mwenyezi Mungu na kwamba Muhammad ni mja Wake na mtume Wake, na kusimamisha Swala…) [ Imepokewa na Bukhari na Muslim.]

2. Swalah ndio amali bora kimatendo.

Amesema Mtume wa Mwenyezi Mungu ﷺ: (Amali bora kuswali mwanzo wa wakati wake). [Imepokewa na Tirmidhi]

3. Swalah ni upambanuzi baina ya Uislamu na ukafiri.

Mtume ﷺ amesema: (Baina ya mtu na ushirikina na ukafiri ni kuacha Swala) [ Imepokewa na Muslim.].

4. Swalah ni nguzo ya Uislamu. Juu yake – baada ya kumpwekesha Mwenyezi Mungu ndio yajenga Uislamu.

Mtume ﷺ: (Kichwa cha jambo hili ni Uislamu na nguzo yake ni Swala) [ Imepokewa na Ahmad].

Fadhila za Swala

1. Swala ni nuru kwa mwenye kuswali. Mtume ﷺ amesema: (Na Swalah ni Nuru) [ Imepokewa na Bukhari na Muslim.].

2. Swala ni kafara ya dhambi. Mwenyezi Mungu Aliyetukuka Amesema: {Na simamisha Swala ncha mbili za mchana na nyakati za usiku zinazokaribiana na mchana. Hakika mema yanafuta maovu. Hayo ni makumbusho kwa wenye kukumbuka} [11: 114].

Na amesema Mtume ﷺ: ( Mnaonaje, lau kuna mto mlangoni mwa mmoja wenu ambao anaoga ndani yake kila siku mara tano, je kutasalia chochote cha uchafu mwilini mwakeWakasema: Hakutasalia uchafu wowote katika mwili wake. Akasema Mtume ﷺ: Huo ndio mfano wa Swala tano,. Mwenyezi Mungu kwa hizo Swalah anayafuta madhambi) [ Imepokewa na Bukhari na Muslim.].

3. Swala ni sababu ya mtu kuingia Peponi. Mtume ﷺ alimwambia Rabi’ah bin Ka’ab, alipomtaka wasuhubiane naye Peponi,: Mtume akamjibu: (Nisaidie kwa kuishughulisha nafsi yako kwa kusujudu sana) [ Imepokewa na Muslim.].

Hukumu ya Swala

Swala tano ni wajibu kulingana na Qur›ani, Sunna na umoja wa wanavyuoni:

1. Qur’ani:

Anasema Mwenyezi Mungu Aliyetukuka: {Na simamisheni Swala na toeni Zaka na rukuuni pamoja na wenye kurukuu} [2: 43].

2. Sunna:

Amesema ﷺ: (Uislamu umejengwa juu ya nguzo tano: kushuhudia kuwa hapana mola isipokuwa Mwenyezi Mungu na kwamba Muhammad ni mja Wake na mtume wake, na kusimamisha Swala, nakutoa Zaka, nakuhiji Alkaba na kufunga mwezi wa Ramadhani) [ Imepokewa na Bukhari na Muslim.].

- Na imepokewa kutoka kwa Twalhah bin ‘Ubeidillah kwamba mtu mmoja alimuuliza Mtume ﷺ kuhusu Uislamu, akasema ﷺ: (Ni Swala tano mchana na usiku. Akasema: “Je, kuna nyingine zinazonilazimu sizizokuwa hizo?” Akasema: La, isipokuwa ukijitolea) [ Imepokewa na Bukhari na Muslim.].

3. Umoja wa wanavyuoni:

Umma kwa umoja wao wamekubaliana juu ya uwajibu wa Swala tano kipindi cha mchana na usiku.

Swala inamlazimu nani?

Swala inamlazimu kila Muislamu, aliyebaleghe, mwenye akili, awe mwanamume au mwanamke.

Kulipa Swala
Kafiri haamrishwi kulipa Swala zilizompita kabla ya kusilimu, kwa kuwa uislamu unafuta yale yaliyo kabla yake.

Hukumu ya mwenye kuacha Swala

1. Mwenye kuacha Swala kwa kukanusha uwajibu wake:

Atafahamishwa akiwa hajui. Akiendelea kukanusha kwake, basi yeye ni kafiri, mkanushaji wa Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na umoja wa Waislamu.

2. Mwenye kuacha Swala kwa uvivu:

Mwenye kuacha Swala kwa kukusudia na uvivu atakuwa amekufuru. Na ni juu ya kiongozi amlinganie kuswali na amuorodheshee toba kwa muda wa siku tatu. Basi akitubia ni sawa, na akitotubia atamuua kwa kuwa ameritadi. Hii ni kwa kauli yake Mtume ﷺ: (Ahadi iliyoko baina ya sisi na wao ni Swala. Yoyote yule atakayeiacha basi atakuwa amekufuru ) [ Imepokewa na Tirmidhi.], na kauli yake ﷺ: (Hakika baina ya mtu na ushirikina na ukafiri ni kuacha Swala) [ Imepokewa na Muslim.].

Swala ya mtoto
Mtoto anaamrishwa kuswali akifika miaka saba, kwa kumzoeza, na anapigwa kwa kuiacha afikapo miaka kumi kipigo kisichoumiza. Amesema Mtume ﷺ: (Waamrisheni watoto wenu kuswali wakiwa ni vijana wa miaka saba, na wapigeni kwa kuiacha swala wakiwa ni vijana wa miaka kumi)) [ Imepokewa na Abu Daud.].