Amekufa Hajafanya Hajj Na Alikuwa Na Uwezo Wa Kufanya Lakini Akapuuzia’ Je, Anaweza Kulipiwa Hiyo Hajj Na Jamaa Zake?

SWALI: Mtu ana uwezo wa kwenda hajj, na ameshapeleka watu kadhaa kwenda hajj ilhali yeye binafsi akiambiwa kwenda, anasema wanaye watamhijia. Ikatokea kweli akafa hajenda hajj, itafaa kumhijia mtu huyu? Ni ipi kauli ya ulamaa juu ya mtu alokuwa na uwezo wa kwenda hajj, lakini akafa hajafanya hajj,yafaa kumhijia? Baaraka Allaahu fiyk

JIBU: AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho. Mtu ambaye hajakwenda Hajj akafariki na alikuwa na uwezo wa kwenda Hajj na akaacha kwa makusudi au kwa kuzembea; wote hao kwa mujibu wa Aqwaal za Ahlul-'Ilm hawahitajii kufanyiwa Hajj hata kama kuna mali zao wameacha zinazotesheleza kufanyiwa Hajj. Japo kuna Wanachuoni wengijne wanaoona kuwa kama kaacha mali anaweza kufanyiwa Hajj kwa mali yake aliyoacha. lakini kauli yenye nguvu ni kutofanyiwa Hajj ya badali (Hajj Al-Badal) kwa sababu kama alikuwa na uwezo na nafasi ya kwenda Hajj na akapuuzia, vipi afanyiwe Hajj na hali mwenyewe hakujali! Huu ni msimamo wa Imaam Ibn Al-Qayyim (Rahimahu Allaah) na kaenda nao Imaam Ibn 'Uthaymiyn (Rahimahu Allaah) ambaye amesema kuwa, kama alikuwa na uwezo wa kufanya Hajj na akapuuzia, basi hakuna Hajj itakayohesabiwa kwake hata kama watu watamfanyia Hajj mara elfu moja. Akaendelea kusema kuwa, hilo linamhusu hata aliyeacha Swawm kwa kupuuzia na hali alikuwa anaweza kufunga, huyo hawezi kulipiwa akifariki kwa sababu aliacha kwa uzembe na kupuuzia. Ama ile Hadiyth ya Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) isemayo, "Yeyote aliyefariki hali ya kuwa anadaiwa Swawm, basi Warithi wake wanapaswa kumfungia." Hadiyth hiyo inamhusu yule ambaye alikuwa hajaacha kufunga kwa kupuuzia. [Fataawa Ibn 'Uthaymiyn (21/226)] Na Allaah ni Mjuzi zaidi




Vitambulisho: