JIBU: Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho. Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu kupata zawadi na kuiuza. Muislamu anapopata zawadi naye akaiuza hilo ni jambo ambalo linakubalika kishari’ah. Hata hivyo inategemea hizo zawadi ulizotaja za serikali na mashirika, je, ni zawadi kwa kucheza au kushiriki mchezo fulani kama bahati nasibu, au unalipa pesa kununua tiketi au bidhaa kwa ajili ya ushiriki wa mashindano ambayo yatakupatia zawadi hiyo? Ikiwa ni hali kati yah ali hizo kwenye maswali yetu hapo juu, basi zawadi hiyo itakuwa haifai kwani itakuwa imeingia kamari na pia ribaa ndani yake. Ama ikiwa ni zawadi tu inayotolewa bila masharti yoyote yale, basi itafaa. Hata hivyo, mas-ala ya kutoa Zakaah ina masharti yake yaliyowekwa na shari’ah. Si yeyote anayetoa Zakaah, japokuwa mtu yeyote anaweza akatoa Sadaqah kwani Sadaqah haina kiwango cha chini. Ikiwa utaiuza hiyo zawadi itategemea utapata kiasi gani. Lau kiasi utakachopata kitafika kiwango cha chini cha kutolewa Zakaah itabidi utoe ikipitiwa na hawl (mwaka wa Kiislamu). Kwa muhsari, ukitekeleza masharti haya mawili itakupasa pesa hiyo uliyopata baada ya kuiuza zawadi kuitolea Zakaah. Masharti yenyewe ni kama yafuatayo: 1. Kuwa na kiwango cha chini kabisa (nisaab) ambacho ni sawa na gharama ya kununua gramu 82 za dhahabu safi. 2. Kiwango hicho kipitiwe na mwaka katika kalenda ya Kiislamu bila ya kupungua. Ikiwa masharti hayo yatatimia basi itabidi akiba yako hiyo uitolee Zakaah. Hata hivyo, katika maisha ya uanafunzi gharama huwa nyingi na wakati mwengine ukahitajika kutumia pesa hizo. Ikiwa utazitumia na ukakosa akiba ya kiwango cha chini basi hutalazimika kutoa Zakaah. Ama kuhusu mama yako hawezi kutoa Zakaah mpaka atimize masharti hayo mawili tuliyoyaandika hapo juu. Ikiwa hizo pesa baada ya kuuza hiyo zawadi utampatia mama yako na iwe imetimiza masharti hayo basi itabidi atoe Zakaah. Na Allaah Anajua zaidi